Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde okoeni huduma za afya Gaza-Wataalamu

Mtoto aliyejeruhiwa, hospitalini, Gaza. Picha ya @UNICEF

Chonde chonde okoeni huduma za afya Gaza-Wataalamu

Afya

Sauti zaidi zimeendelea kupazwa ili kunusuru huduma za afya kwenye ukanda wa Gaza huko Mashariki ya Kati wakati ambapo idadi ya wasaka huduma ni kubwa, ilhali watoa huduma, vifaa vya tiba na maeneo ya kutoa huduma siyo tu hayatoshelezi bali pia vimesambaratika.

Wataalamu maalum wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michael Lynk na Dainius Pūras  wamepaza sauti hizo wakiungana na makundi mengine ambayo nayo awali yalitaka hatua zaidi zichukuliwe ili kunusuru huduma hizo za afya.

“Tuna hofu kubwa kutokana na ripoti za uhakika zinazosema ya kwamba kutibu na kuhudumia maelfu ya majeruhi waliotokana na mashambulizi ya risasi kutoka jeshi la Israeli ya miezi mitatu sasa kumezidi uwezo wa mfumo wa afya wa Gaza,” wamesema wataalamu hao katika taarifa yao ya pamoja waliyotoa leo huko Geneva, Uswisi.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, takribani waandamanaji 8,000 wa huko Gaza wamelaza hospitali ambapo zaidi ya 3,900 kati yao walijeruhiwa kwa silaha za moto.

Idadi kubwa yaelezwa wana majeraha ya kudumu ikiwemo kukatwa viungo vyao.

“Ambacho hakikubaliki ni kwamba wale wanaohitaji huduma ambayo hivi sasa haipo Gaza, wamenyimwa vibali vya kutoka ili waweze kupata huduma nje ya Gaza,” wamesema wataalamu hao.

Wataalamu hao wameikumbusha Israel ambayo inakalia eneo hilo, kuwa ina wajibu wa kulinda wakazi wa Gaza na kuhakikisha ustawi wao, pamoja na kuruhusu na kuwezesha huduma za afya zinazohitajika.

Kwa mujibu wa wataalamu hao, changisho la zaidi ya dola milioni 6 kukidhi baadhi ya mahitaji ya dharura limepatikana, bado dola milioni 13 zinahitajika .

Fedha hizo pamoja na mambo mengine zitawezesha kupelekwa kwa jopo la dharura la wataalamu wa afya na kununua dawa muhimu sambamba na kusaidia huduma za kurejesha watu katika hali ya kawaida.

“Kiwango hicho ni sehemu ndogo sana ya zaidi ya dola milioni 500 zilizoombwa kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya kibinamu kwenye ukanda wa Gaza na maeneo mengine ya Palestina  yanayokaliwa,” wamesema wataalamu hao wakisihi jamii ya kimataifa ionyeshe ukarimu zaidi.