Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fedha za wahamiaji hukwamua nchi zao za asili- UNCTAD

Lundo la fedha za kisomali katika mitaa ya Mogadishu, Somalia.Mamilioni ya watu kwenye nchi hiyo ya pembe ya Afrika hutegemea zaidi fedha zinazotumwa na ndugu zao waishio ughaibuni.
AU-UN IST/Stuart Price

Ukuaji wa Kiuchumi

Ingawa wanaishi ughaibuni, wahamiaji bado wanachangia kiuchumi kwenye nchi walizotoka. Nchi hunufaika, halikadhalika familia zao.

Kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD, imesema fedha zinazotumwa na wahamiaji walioko ughaibuni zimekuwa mkombozi kwa mataifa mengi ya Afrika.

Mathalani kati ya mwaka 2014 na 2016 wahamiaji walioko ughaibuni walituma jumla ya dola bilioni 65 kwa nchi za Afrika.

Afisa katika ofisi ya UNCTAD, huko Geneva, Uswisi, Jane muthumbi akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa ametaja baadhi ya nchi nufaika zaidi ikiwemo Liberia ambayo asilimia 27 ya pato la nchi hutokana na fedha zinazotumwa na wahamiaji.

Wahamiaji, kama huyu anayefanya kazi nchini Jordan, hutuma fedha kwenye nchi zao za asili, fedha ambazo hunufaisha siyo tu nchi zao bali pia familia zao.
IRIN/Maria Font de Matas
Wahamiaji, kama huyu anayefanya kazi nchini Jordan, hutuma fedha kwenye nchi zao za asili, fedha ambazo hunufaisha siyo tu nchi zao bali pia familia zao.

Halikadhalika Gambia mwaka jana asilimia 21 ya pato la ndani na  Comoro asilimia 20 ya pato la nchi lilitokana na utumwaji wa fedha.

Hata hivyo amesema kiwango kinachotumwa kingaliweza kuwa kikubwa zaidi iwapo gharama za kutuma na kupokea fedha kutoka ughaibuni ingalipunguzwa. Kwa hivyo amesema hatua muhimu ni kupunguza gharama kwa mujibu wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Amesema kwa mujibu wa SDGs, gharama hiyo inapaswa kupunguzwa kwa asilimia 3.