Bado ukata waathiri wakimbizi na wenyeji Uganda- UNHCR

20 Juni 2018

Uganda yafungua milango kwa wakimbizi, wahisani nao wasuasua kufungua pochi zao ili kusaidia operesheni za usaidizi.

Nchini Uganda nako maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani yamefanyika kwenye makazi ya wakimbizi ya Nakivale, wilayani Isingiro, kwenye nchi hiyo ambayo imefungua milango yake kwa ajili ya wakimbizi kutoka nchi kadhaa zikiwemo Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Hata hivyo ufadhili wa fedha kwa ajili ya kuhudumia wakimbizi hao unasuasua ambapo Mwakilishi mkazi wa shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa nchini Uganda, Boutroue Joel akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa wakati wa maadhimisho hayo amesema kati ya dola milioni 450 zilizoombwa, wamepokea asilimia 25 pekee.

Amesema kwa mantiki hiyo operesheni zao za kusaidia wakimbizi zinaathirika akisema..

Sauti ya Boutroue Joel 

 “Kutakuwepo na sitisho kwenye mgao wa chakula, kadri WFP inahusika. Kwa upande wetu hatuwezi kujenga shule za kutosha au kuajiri walimu wa kutosha. Hatuwezi kujenga au kukarabati vituo vya afya, makali yanawapata moja kwa moja wakimbizi na jamii zilizowahifadhi kwa sababu tusisahau tuliahidi kusaidia pia  jamii hizo na wakimbizi.  Wahisani wanatoa ahadi na kwa kawaida wanaweza kukamilisha ahadi ambazo hatimaye hazitoshelezi.”

Ameomba msaada zaidi ili waweze kuongeza huduma zao za kibinadamu kwa wakimbizi akitolea mfano kujenga shule na kuandikisha watoto zaidi kwa kuwa elimu ni moja ya haki ya msingi ya mtoto.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud