Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto hawapaswi kutenganishwa na familia licha ya hali ya uhamiaji-UNICEF

Noor na Sarah wakitembea magharibi mwa Mosul ambako majengo mengi yaliharibiwa.
UNICEF/UN0161148/Rfaat
Noor na Sarah wakitembea magharibi mwa Mosul ambako majengo mengi yaliharibiwa.

Watoto hawapaswi kutenganishwa na familia licha ya hali ya uhamiaji-UNICEF

Haki za binadamu

Taarifa ya kwamba watoto wakiwemo wachanga wanatenganishwa na wazazi wao wakati wanatafuta usalama nchini Marekani zinaumiza moyo, limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF.

Shirika hilo limesema watoto bila kujali wanatoka wapi au hali yao ya uhamiaji ni watoto kwanza kabisa na wale walioachwa bila chaguo lakini kukimbia makazi yao wana haki ya kulindwa, kupata huduma muhimu, na kuwa na familia zao kama watoto wote.

Zaidi ya yote limesema ni muhimu kutambua haki hizo ambazo humpa kila mtoto fursa bora katika maisha ya baadaye yenye furaha.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, msemaji wa UNICEF Christophe Boulierac, amesema kuzuiliwa na kutenganishwa na familia huenda kukaleta msongo wa mawazo amabao huenda ukaweka watoto katika hatari zaidi.

Boulierac amesema vitendo hivyo havizingatii maslahi ya mtu yeyote, hususan watoto ambao wengi wanaathirika zaidi akiongeza kuwa usalama wa watoto unapaswa kupewa kipaumbele

"Kwa miaka mingi, serikali ya Marekani na watu wake wameunga mkono jitihada zetu za kusaidia wakimbizi watoto, wanaotafuta hifadhi na wahamiaji walioathirika na migogoro duniani kote.Iwapo ni vita huko Syria au Sudan Kusini, njaa nchini Somalia, au tetemeko la ardhi huko Haiti, Marekani imekuwa tayari kusaidia, na kukaribisha watoto waliofurushwa makwao.Natumaini kwamba maslahi bora ya wakimbizi na watoto wahamiaji itakuwa kipaumbele katika taratibu na sheria za kuomba uhifadh,” amesema Bwana Boulierac.