Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afya ya wakazi Yemen inategemea bandari ya Hudaidah -WHO

 Mlolongo wa magari  yakisubiri kupita katika daraja liloshambuliwa.Barabara hii ni moja wa zile zinazounganisha Hodeida(Al Hudayda) na sehemu zingine za nchi.
OCHA/Giles Clarke
Mlolongo wa magari yakisubiri kupita katika daraja liloshambuliwa.Barabara hii ni moja wa zile zinazounganisha Hodeida(Al Hudayda) na sehemu zingine za nchi.

Afya ya wakazi Yemen inategemea bandari ya Hudaidah -WHO

Afya

Kuendelea kwa mapigano mjini Hudaidah nchini Yemen kunahatarisha wakazi ambao ni waathirika wa moja kwa moja na asilimia 70 ya watu wanaotegemea huduma muhimu ikiwemo, huduma ya afya inayopita bandari iliyomo mjini humo.

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limesema linasimama pamoja na wadau wa Umoja wa Mataifa kutolea wito pande husika katika mzozo kuhakikisha kuwa bandari ya Hudaidah inasalia wazi na kazi ikifanyika kwani ni uti wa nchi nzima.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi msemaji wa WHO Christian Lindmeier amesema bandari ya Hudaidah ni muhimu kwa ajili ya kuingizia bidhaa muhimu za kukabiliana na kipindupindu na kuhara kwani asilimia 70 ya vifaa muhimu ikiwemo vifaa vya matibabu huingia Yemen kupiitia bandari hiyo.

Wakati watu milioni 8.4 wakikabiliwa na hali ya ukame na wakitegemea msaada wa kibinadamu, WHO imetolea wito pande kinzani kulinda watoa huduma wa afya, vituo vya afya na miundombinu ikiwemo vituo vya maji.
(Sauti ya Christian Lindmeier)

“WHO imepeleka wafanyakazi 15 wa dharura kwa ajili ya kutoa huduma za msongo wa mawazo na huduma nyingine zinazohitajika, ni wafanyakazi wachache tu wamesalia Hudaidah, tunawapongeza kwa kazi nzuri na kujituma katika kulinda  afya ya watu wa Hodeida.”
 WHO imeweka vituo vya kukabiliana na majeruhi, vituo vya kutibu kipindupindu na watoto wanaokabiliwa na changamoto mbali mbali za kiafya.