Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waliofurushwa makwao 2017 pekee ni sawa na idadi ya watu wa Thailand -UNHCR

Mtoto mvulana akiwa pekupeku ambaye ndio amewasili tu kwenye kambi ya wakimbizi ya Kakuma Kaskazini Magharibi mwa Kenya kutokea Sudan Kusini akiwa na sanduku lake kichwani akijaribu kuwahi utaratibu wa kuandikisha wakimbizi
OCHA/Gabriella Waaijman
Mtoto mvulana akiwa pekupeku ambaye ndio amewasili tu kwenye kambi ya wakimbizi ya Kakuma Kaskazini Magharibi mwa Kenya kutokea Sudan Kusini akiwa na sanduku lake kichwani akijaribu kuwahi utaratibu wa kuandikisha wakimbizi

Waliofurushwa makwao 2017 pekee ni sawa na idadi ya watu wa Thailand -UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Watu milioni 68.5 walikuwa wamefurushwa kutoka makwao hadi mwishoni mwa mwaka 2017, imesema ripoti mpya ambayo imetolewa leo huko Geneva, Uswisi na shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR.

Ripoti hiyo ya UNHCR kuhusu mwenendo wa wakimbizi, inasema idadi hiyo inajumuishawakimbizi  waliotoroka nchi zao mwaka jana wakikimbia migogoro pamoja na unyanyasaji ambao ni milioni 25.4, idadi ambayo ni sawa na idadi ya watu wa Thailand.

Kiwango hicho ni ongezeko la watu milioni 2.9 ikilinganishwa na mwaka 2016. idadi ambayo pia ni kubwa kuwahi kushuhudiwa na UNHCR kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Wakimbizi wa Syria nje ya makazi yao kufuatia dhoruba kali la  theluji iliyoleta mvua.
Picha ya UNICEF/UNO158355/Halidorsson
Wakimbizi wa Syria nje ya makazi yao kufuatia dhoruba kali la theluji iliyoleta mvua.

 

Akizungumza na waandishi habari mjini Geneva, Kamishna Mkuu wa wakimbizi , Filippo Grandi ametaja sababu za ongezeko hilo.

 (SAUTI YA FILIPPO GRANDI)

“ Hii ni kwa sababu ya kuendelea kwa migogoro,  kushindwa kutafutia dawa migogoro hiyo inayoendelea, wananchi kuendelea kushinikizwa katika mataifa yaliyo na migogoro ambayo inawalazimisha kuacha makazi yao, na migogoro mipya kama ule wa warohingya, ambao  unahusika katika kusababisha ongezeko la idadi ya wakimbizi.”

Ripoti inasema pia kuwa idadi ya wakimbizi wapya nayo inazidi kuongezeka ambapo katika mwaka wa 2017 pekee watu milioni 16.2, huenda walikimbia kwa mara ya kwanza au wamekimbia tena makwao.

Watu 25.4 milioni walihama makwao mwaka 2016 kutokana na migogoro na unyanyasaji

Hii ina maana kuwa kila sekunde, kwa wastani, mtu mmoja anapoteza makazi.

Kwa ujumla  mataifa yanayoendelea ndiyo yanaathirika mno.

Kamishna Mkuu Grandi, amezitaja baadhi ya nchi ambazo kuna idadi kubwa ya wakimbizi.

(SAUTI YA FILIPPO GRANDI)

 “Venezuela ina idadi kubwa ya watu  wanaohitaji ulinzi kwani watu milioni moja na nusuwalitoroka nchi yao katika kipindi cha miaka michache iliyopita, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na mataifa mengine. Kwa hivyo, maeneo machache ambayo yalikuwa na matatizo madogo lakini sasa shida zinaongezeka, na mengine hayana ishara ya kupungua na kwa hivyo watu hawarejei makwao na kwa hivyo ongezeko la watu wasio na makazi.”

Ripoti inamnukuu mkimbizi mmoja, mwenye umri wa miaka 55 Mutaybatu, akisema kuwa  walitembea kwa siku 10 na baadaye kuvuka mto kwa kutumia boti.

Akizungumza kutoka katika makazi ya wakimbizi warohingya huko Bangladesh, amesema kuwa safari ilikuwa ngumu, bila chakula na kuna wakati walikula majani.