Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IMF lazima ibadilike ili iwe na tija kwa maskini- Mtaalamu

Makao makuu ya shirika la fedha duniani la IMF  mjini Washington, DC Marekani
Picha ya IMF/Henrik Gschwindt de Gyor
Makao makuu ya shirika la fedha duniani la IMF mjini Washington, DC Marekani

IMF lazima ibadilike ili iwe na tija kwa maskini- Mtaalamu

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la fedha duniani, IMF halina maadili ya kutosha ya kuweza kulinda mataifa ya kipato cha chini, amesema mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu umaskini uliokithiri na haki za binadamu.

Mtaalamu huyo Philip Alston ametoa kauli hiyo leo mjini Geneva, Uswisi wakati akiwasilisha ripoti yake mbele ya kikao cha Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa.

IMF inapaswa kuchukua hatua kuokoa wananchi wa kipato cha chini ambao wanabeba mzigo wa sera za kupunguza matumizi zinazotekelezwa na serikali kwa maelekezo ya shirika hilo,”amesema Bwana Alston.

Amesema kuchukua hatua kusaidia watu ambao ni mafukara bado kumesalia jambo lisilotiliwa maanani na shirika hilo kwenye majukumu yake duniani kote.

Image
Msemaji wa IMF Gerry Rice akizungumza na waandishi wa habari huko Washington DC nchini Marekani. Picha: UM/Video capture

 

Mtaalamu huyo amesema iwapo IMF itazinduka na kuamua kuchukua hatua kulinda makudni hayo, basi shirika hilo linahitaji mtazamo mpya tofauti na ule wa sasa.

“IMF ni mtendaji mkuu mwenye ushawishi mkubwa kwenye jukwaa la kimataifa, siyo tu kwenye masuala ya sera za kifedha bali pia kwenye masuala ya ulinzi wa kijamii. Hata hivyo licha ya kauli za kuvutia za Mkurugenzi wake mtendaji Christine Lagarde, bado hakuna utekelezaji wa ahadi hizo,” ameongeza mtaalamu huyo.

Bwana Alston ametaka shirika hilo liache kulenga masuala ya hifadhi ya kijamii pindi linaposaka kupunguza matumizi ya serikali, kwani hatua hiyo huathiri zaidi maskini wa kupindukia.

Ubongo mkubwa na maadili kidogo

Amesema ushahidi ni dhahiri kuwa hatua hizo za kubana matumizi huishia kuwaumiza maskini na kuwa na manufaa kwa watu wenye maisha bora zaidi.

Mtaalamu huyo amefananisha shirika hilo na kitu chenye ‘ubongo mkubwa  na maadili kidogo’ hivyo ni lazima ijifunze na makosa yaliyopita ili kubadilika.

Mathalani ametaja mabadiliko hayo kuwa ni pamoja na kuajiri watu kutoka maeneo mbalimbali na wenye mtazamo tofauti ili kubadilisha mtazamo na fikra wa shirika hilo.

Kwa mujibu wa Bwana Alstona, kwa wastani mfanyakazi wa IMF ni mchumi kutoka nchi za magharibi aliyesoma katika vyuo vya hali ya juu penginepo Marekani au Uingereza.

“Shirika hili haliwezi kubadilika bila kubadili wafanyakazi wake,” amehitimisha mtaalamu huyo maalum.