FAO yachukua hatua kupunguza madhara ya maafa Tanzania
Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO, limeanza kuwajengea uwezo wataalamu wa kuandaa mipango ya kukabili maafa nchini Tanzania kama njia mojawapo ya kupunguza maafa.
Mipango hiyo inatekelezwa kwa kushirikiana na ofisi ya Waziri Mkuu nchini humo ambapo awamu ya kwanza imeanza kutekelezwa mkoani Kagera kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.
Halmashauri zinazonufaika ni pamoja na Bukoba na Misenyi ambapo awamu ya pili inatarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi ujao.
Julius Sonoko ambaye ni mratibu wa FAO mkoani Kagera, amesema kuwa wanatoa mafunzo maalumu kwa kamati za maafa ambazo zinajadili taarifa zilizokusanywa hasa kwenye wilaya za Misenyi na Bukoba mkoani Kagera, ili kuwezesha kufikisha uelewa kwa wananchi watakaoweza kutoa ushirikiano wakati wa utekelezaji wa mpango husika.
Bwana Sonoko ambaye ni mratibu wa FAO mkoani Kagera, anafafanua zaidi mpango huo.
Sauti ya Julius Sonoko
Mpango huu wa FAO unaolenga kaya elfu tano, unafuatia maafa ya tetemeko la ardhi mkoani Kagera ambalo lilisababisha vifo, likaharibu makazi na mazao pamoja na kuwaacha wananchi , hasa wanaotegemea kilimo bila ya kuwa na namna ya kupata mahitaji yao ya kila siku.