Watoto waliozaliwa baada ya mama zao kubakwa vitani wana haki: Guterres

19 Juni 2018

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kutokomeza ukatili wa kingono kwenye mizozo, Umoja wa Mataifa mwaka huu unataka watoto waliozaliwa kutokana na ukatili wa kingono vitani watendewe haki.

Katibu Mkuu Antonio Guterres katika ujumbe wake amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa mara nyingi watoto wanaozaliwa kutokana na vitendo vya  ubakaji wakati wa migogoro hukabiliwa na tatizo la utambulisho katika jamii.
Amesema tatizo hilo hudumu nalo maisha yao yote hata baada ya vita na mara nyingi mama zao hutengwa na kulaumiwa na  jamii zao.
Madhila wanayokumbana nao wazazi na watoto hao yameshuhudiwa na mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili wa kingono vitani, Pramila Patten aliyepata fursa ya kuzungumza na wakimbizi wanawake wa Rohingya huko Bangladesh waliokumbwa na ubakaji.
Akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa  Mataifa Bi. Patten amesema..

 Sauti ya Pramila Patten
Wanaogopa kupuuzwa na jamii ya  kimataifa. Wanataka haki: huo ndio ujumbe nilioupata kutoka kwa wengi kwa siku moja niliyokuwepo kambini. Wanataka wahalifu wafikishwe mbele ya sheria, na wanaelewa sana kinachoendelea sasa, na walinipatia taarifa zote; ya kwamba mauaji ya kimbari yanaendelea dhidi ya watu wao na wanataka ulimwengu mzima ufahamu hivyo.
 
Bi. Patten akazungumzia msaada unaotolewa kwa wanawake wajawazito na watoto waliozaliwa kutokana na vitendo vya ubakaji katika migogoro ya kivita.

Sauti ya Pramila Patten
Nadhani bado kuna kazi zaidi ya kufanya.. Lakini kinachofurahisha ni kwamba kwamba tatizo hilo  linashughulikiwa na UNICEF. Lakini nadhani kama mtoto aliyezaliwa kutokana na ubakaji ametelekezwa, au amewekwa katika taasisi, au anatunzwa na  jamii, nadhani unyanyapaa aliopitia utabaki palepale. Wasiwasi wangu pia unahusiana na usajili wa uzazi kwa sababu nadhani kuna masuala mapana ya utambulisho wa kijamii na utambulisho wa kisheria.

Na je  jamii ya wakimbizi kambini hususan wanaume, wanawachukuliaje wanawake au wasichana waliopitia madhila ya ubakaji?
Sauti ya Pramila Patten
Kwa mfano, wote wameripoti, hususan wale walio hatarini zaidi: wanawake viongozi wa kaya au wale wenye barubaru wa kike, wamekuwa wanalalamika kuhusu unyanyasaji na ukatili. Nilipata ripoti za matukio mengi ya wanaume kutoka katika jamii hiyo kupenya kwenye mahema na kuingia kwenye makazi nyakati za usiku .

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud