Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania iko mbele kujumuisha watu wenye ulemavu kwenye SDGs

Ikupa Stella Alex, Naibu Waziri wa Nchi ofisi  ya Waziri Mkuu nchini Tanzania anayehusika na masuala ya watu wenye ulemavu katika mahojiano na UN News kandoni mwa mkutano wa mkataba wa haki za watu wenye ulemavu, New York
UN News/Assumpta Massoi
Ikupa Stella Alex, Naibu Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu nchini Tanzania anayehusika na masuala ya watu wenye ulemavu katika mahojiano na UN News kandoni mwa mkutano wa mkataba wa haki za watu wenye ulemavu, New York

Tanzania iko mbele kujumuisha watu wenye ulemavu kwenye SDGs

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Tanzania imetaja hatua ambazo inachukua ili kuhakikisha watu wenye ulemavu hawaachwi nyuma katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Naibu Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu nchini humo anayehusika na masuala ya walemavu, Ikupa Stella Alex ametaja hatua hizo alipozungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Amesema wamekuwa wakijitahidi kutenga fedha kwa ajili ya kununua vifaa ya kujifunzia na kufundishia kwa watu wenye ulemavu.  Halikadhalika vifaa saidizi kama vile viti mwendo na mafuta kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa ngozi. "Tumekuwa tukisisitiza kuwa kila halmashauri inapoagiza dawa kutoka Bohari ya Dawa, ni lazima ijumuishe mafuta ya watu wenye ulemavu wa ngozi, na mafuta haya yanatolewa bure," amesema Naibu Waziri huyo.

Bi. Alex pia amesema wanajitahidi kuhakikisha kuwa kuna walimu wanaotosheleza kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum.

Akaenda mbali zaidi kuzungumzia miundombinu kwenye shule akisema kuwa, " Sasa hivi tumekuwa tukifanya maboresho kwa shule zetu kongwe. Tumekuwa tukijitahidi sana kwani awali miundombinu haikuwa rafiki. Kwa hiyo hivi sasa katika ukarabati tunazingatia hilo. Lakini katika majengo yanayojengwa sasa hivi au shule ni lazima mtu ahakikishe kuwa ina miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu."

Ameongeza kuwa wanasisitiza kuwa ni lazima kwenye shule kuna choo ambacho ni rafiki kwa wanafunzi wenye ulemavu.