Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusiwaonee haya wanaolaghai wazee kifedha- Mtaalamu

UN Photo/Logan Abassi
Nyumba ya wazee. Picha:

Tusiwaonee haya wanaolaghai wazee kifedha- Mtaalamu

Haki za binadamu

Vitendo vya kulaghai wazee hadi wanakubali kukabidhi fedha au mali zao kwa wale wanaowahudumia vimeshamiri ingawa takwimu za ukubwa wa tatizo hilo bado haziko bayana kutokana na watu kunyamazia ukatili huo.

 

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za wazee Rosa Kornfeld-Matte amesema hayo leo kuelekea siku ya kuelimisha umma kuhusu ukatili dhidi ya wazee hapo kesho.

Amesema mara nyingi wazee hujikuta wakilaghaiwa hadi kuwapatia fedha watu ambao wanawahudumia, tatizo ambalo amesema linatarajiwa kuongezeka wakati huu ambapo idadi ya wazee inatarajiwa kuongezeka.

Bi.Kornfeld-Matte amesema cha kusikitisha zaidi walaghai hao ni wanafamilia na ndugu wa karibu na ni kwa mantiki hiyo inakuwa vigumu kuwaripoti kwenye vyombo vya sheria kwa hofu ya kuleta aibu kwenye ukoo na pia kusitishwa kwa huduma.

Halikadhalika anasema inakuwa ni vigumu kutofautisha iwapo ni kitendo cha ulaghai au upendo pindi mzee anapohamisha fedha au mali zake kwenda kwa mtu anayemhudumia.

Hata hivyo amesema moja ya mbinu bora za kudhibiti tabia hiyo ni kuweka kando hoja ya aibu na kuripoti vitendo hivyo kwenye mamlaka ya sheria.

Ametoa wito kwa jamii kupaza sauti zao pindi wanapohisi au wanaposhuku ukatili wa aina hiyo dhidi ya mzee.