UN yataka ulinzi kwa wapalestina

Wanachama wa Umoja wa Mataifa wamepitisha azimio la kutaka ulinzi kwa raia wa Palestina.
Wajumbe wa Baraza Kuu la umoja huo wamepitisha azimio hilo kwa kura 120 huku kura 8 zikisema hapana na wajumbe 45 hawakupiga kura.
Rasimu ya muswada iliwasilishwa na Algeria, Uturuki pamoja na Palestina kufuatia makabiliano kati ya wa Palestina na vikosi vya Isreal ambavyo vililaumiwa kwa kutumia risasi za moto dhidi ya waandamanaji.
Muundo wa rasimu hii unadhihirisha kuwa siasa ndio inatawala hapa
Mwanzo rasimu hiyo ilipata pingamizi kutoka kwa Marekani ambayo ilitaka kuwekwe kipengele kinacholaani kundi la Hamas na pia kutaka kundi hilo libebeshwe mzigo wa lawama za vurugu.Mwakilishi wa kudumu wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Balozi Nikki Haley, alitetea kipengele hicho.
(SAUTI YA NIKKI HALEY)
“Muundo wa rasimu hii unadhihirisha kuwa siasa ndio inatawala hapa. Rasimu yenyewe inaegemea upande mmoja tu. Kamwe haitaji popote kundi la Hamas ambalo kila mara huchochea ghasia katika eneo la Gaza.”
Licha ya kampeni hiyo, akisaidiwa na Israel kutoa hoja, hilo halikuwageuza wajumbe ambao walikuwa wanajiandaa kupiga kura. Kura yenyewe ilihusu ikiwa kifungu hicho, cha ziada , kiwepo katika rasimu hiyo au la.
(SAUTI YA RAIS WA BARAZA)
“ Matokeo ni kama ifuatavyo: wanaounga mkono 62, wanaopinga 58 na wale hawakupiga 42”
Hivyo kifungu cha Marekani kikaondolewa jambo ambalo Marekani ilikata rufaa. Hii ni kwa sababu japo wanaounga mkono walikuwa wengi 62 na wa hapana 58, lakini azimio halikupata theluthi mbili ya kura inayohitaji ili kupita. Ingawa Marekani ilitaka kuwa kura ipitishwe kutokana na hoja ya ushindi mdogo,hilo lilikataliwa na kupiga tena kura.
Marekani ikashindwa.
Matokeo yalikuwa waliounga mkono rufaa ya Marekani walikuwa 66 huku waliioipinga kuwa 72 na wajumbe 42 hawakupiga kura. Hivyo, kwa mara nyingine, Marekani ikashindwa.
Hatimaye katika rasimu ya kutaka raia wa Palestina kulindwa dhidi ya nguvu za kupindukia za Israel, Matokeoyalionyesha kama ndio walipata kura za kishindo 120, 8 za hapana na waliokata kupiga walikuwa 45.
Rasimu ilichochewa na ghasia za hivi majuzi katika Gaza baada ya Marekani kuhamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem jambo lilozusha maadamano eneo la Gaza na kupelekea vifo vya watu 40 na wengine 5,511 kujeruhiwa.