Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano ya kudhibiti Hudaydah yapamba moto, UN yazungumza

Wakimbizi waliokimbia mapigano nchini Yemen.(Picha:OCHA)

Mapigano ya kudhibiti Hudaydah yapamba moto, UN yazungumza

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi wake kuhusu mapigano yanayoendelea kwa lengo la kudhibiti bandari ya Hudaydah nchini Yemen, bandari ambayo ni tegemeo kwa ajili ya kufikisha misaada ya kibinadamu nchini  humo.

Vyombo vya habari vinaeleza kuwa majeshi yanayounga mkono serikali inayotambuliwa kimataifa yakisaidiwa na Saudi Arabua wanashambulia bandari hiyo ya Hudaydah ambayo kwa sasa inashikiliwa na wahouthi wanaodaiwa kusaidiwa na Iran.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Yemen Martin Griffiths amesema mapigano zaidi kwenye eneo hilo yatakuwa na madhara makubwa kwenye hali ya kibinadamu pamoja na kuzorotesha mashauriano ya kisiasa.

Kupitia taarifa yake iliyotolewa leo mjini New York, Marekani, Bwana Griffiths amesema hakuna suluhu ya kijeshi kwenye mzozo huo.

Mjumbe huyo amesema “tunaendelea kutumia kila fursa kuepuka mapigano zaidi mjini Hudaydah. Tunaendelea na mawasiliano na pande zote husika ili kuwa na mipango kuhusu Hudaydah ambayo itashughulikia hofu za kisiasa, kibinadamu, kiusalama za pande zote husika.”

Ametoa wito kwa pande hizo kushiriki kwa dhati kwenye juhudi za kuepusha mashambulizi zaidi ya kijeshi dhidi ya mji huo.

“Natoa wito pia kwa pande  hizo kujizuia na hatua zaidi za kijeshi na badala yake kupatia amani fursa. Umoja wa Mataifa umeazimia kusongesha mbele mchakato wa kisiasa licha ya matukio ya hivi karibuni,” amesema Bwana Griffiths akisema kuwa umoja huo pia umeazimia kwa dhati kufikia suluhu ya kisiasa na kumaliza mgogoro nchini Yemen.