Zaidi ya wahamiaji milioni 2.5 walisafirishwa kimagendo 2016- UNODC

Utafiti kutoka ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kudhibiti madawa ya kulevya na uhalifu, UNODC, umebaini kuwa zaidi ya wahamiaji milioni 2.5 walisafirishwa kimagendo mwaka 2016.
Biashara hiyo haramu iliwaingizia wasafirishaji hao kipato cha dola bilioni 7, kiwango ambacho kilitumiwa na Marekani au nchi za Ulaya kwa ajili ya usaidizi wa kibinadamu mwaka 2016.
Watoto wanaosafiri peke yao au waliotenganishwa na wazazi wao walikuwa ni miongoni mwa wahamiaji waliolaghaiwa na kusafirishwa au kukumbwa na ukatili, ikielezwa kuwa katika kipindi hicho watoto 34,000 wa aina hiyo waliwasili Ugiriki, Italia, Bulgaria na Hispania.
Utafiti umetaja njia kuu 30 ikiwemo bahari ya Mediteranea ambazo hutumiwa kusafirisha wahamiaji kimagendo na kubaini kuwa mahitaji ya safari za aina hiyo ni kubwa kwa wakimbizi ambao, kutokana na shida wanahitaji kutumia wasafirishaji wa kimagendo ili kukimbia makwao.
Jean Luc Lemahiew ambaye ni mkurugenzi wa sera na masuala ya kisiasa wa UNODC, amesema uhalifu huo unafanywa kwenye mgongo wa watu ambao hawawezi kujitetea kwa lolote , hivyo kunahitajika mikakati ya kikanda na ya kimataifa ili kukabiliana na magenge wa wahalifu hao kwa kuwafikisha katika vyombo vya sheria .
Kwa mujibu takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, maelfu ya wahamiaji hufariki dunia katika harakati hizo za kusafirishwa kimagendo. Wengi wao hufa kwa kuzama baharini, huku wengine wakipoteza maisha kwenye ajali au mazingira magumu ya hali ya hewa.
Usafirishaji wahamiaji kimagendo huhusisha mifumo ya hali ya juu ikiwemo ndoa za kupanga, ajira na nyaraka bandia au kuwapa rushwa maafisa waandamizi.
UNODC inasema kuchagiza uelewa kwenye jamii ambako wahamiaji hao wanatoka hususan kwenye kambi za wakimbizi kuhusu hatari zinazohusiana na mwenendo huo wa usafirishaji binadamu kimagendo kutaweza kusaidia kupunguza mahitaij ya huduma hizo.