Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yaunga mkono mazungumzo kati ya viongozi wa Marekani na DPRK

Rais wa Marekani Donald Trump (kulia) alipokutana na Kim jong-un wa DPRK Singapore
White House (ikulu)
Rais wa Marekani Donald Trump (kulia) alipokutana na Kim jong-un wa DPRK Singapore

UN yaunga mkono mazungumzo kati ya viongozi wa Marekani na DPRK

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umekaribisha kufanyika kwa mkutano kati ya viongozi wa Marekani na Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK huko Singapore.

Katibu Mkuu wa umoja huo, Antonio Guterres ametaja hatua hiyo ni muhimu katika kusongesha amani endelevu na kufanikisha kuondokana na nyuklia kwenye rasi ya Korea kwa njia ambayo itathibitishwa.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa kupitia barua ambayo Bwana Guterres aliandika kwa viongozi hao Donald Trump wa Marekani na Kim Jong Un wa DPRK, kabla ya mazungumzo, aliwaeleza kuwa mwelekeo utahitaji ushirikiano, kulegeza misimamo na kuwa na nia moja.

Amesema kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa awali na ya sasa kwa mujibu wa maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kutahitaji uvumilivu na uungwajii mkono wa kimataifa.

 Bwana Guterres amesihi pande zote husika kutumia fursa ya sasa na amesisitiza utayari wake wa kuunga mkono mchakato unaoendelea.

IAEA NAYO YAKARIBISHA MATOKEO YA MKUTANO KATI YA MAREKANI NA DPRK

Wakati huo huo shirika la kimataifa la nishati ya Atomiki, IAEA limekaribisha taarifa ya pamoja kati ya Rais Donald Trump wa Marekani na Kim Jong Un wa Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK.

Taarifa hiyo inaonyesha azma ya DPRK ya kuondoa kabisa nyuklia kwenye rasi ya Korea.

Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Yukiya Amano kupitia taarifa yake aliyoitoa mjini Vienna Austria, pamoja na kupongeza taarifa hiyo amesema watafuatilia kwa makini mazungumzo kati ya nchi mbili hizo yenye lengo la kutekeleza matokeo ya mkutano wa leo.

Ameongeza kuwa IAEA iko tayari kufanya shughuli zozote za uhakiki huko DPRK ambazo itaombwa kufanya na mataifa yoyote husika, kwa idhini ya bodi ya magavana wa IAEA.