Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Upasuaji wa midomo sungura CCBRT umebadili maisha yangu:Agnes

Binti wa miaka 15 kutoka tanzania, anasema upasuaji wa kurekebisha mdomo sungura umebadili maisha yake
CCBRT/Dieter telemans
Binti wa miaka 15 kutoka tanzania, anasema upasuaji wa kurekebisha mdomo sungura umebadili maisha yake

Upasuaji wa midomo sungura CCBRT umebadili maisha yangu:Agnes

Afya

Wakati mkutano wa kimataifa wa watu wenye ulemavu ukianza leo kwenye makao makuu ya umoja wa Mataifa hapa New York Marekani, nchini Tanzania hospitali ya CCBRT yafufua matumaini ya maisha kwa wenye ulemavu.

Kutana na msichana Agnes, kutoka Kusini Magharibi mwa Tanzania, alitelekezwa na baba yake alipozaliwa tu  na kwa miaka 15 amekuwa akiishi na jinamizi la kutokubalika na jamii yake, kisa jinsi anavyoonekana.

Agnes alizaliwa na ulemavu ujulikanao kama mdomo sungura au (cleft lip) na baba yake hakuweza kuhimili kuishi na mtoto aliyemuona si wa kawaida hivyo akaondoka, na kibarua kikasalia kwa mama yake ambaye alijaribu kila njia kupata matibabu kwa binti yake bila mafanikio kisha akakata tamaa.

Lakini mwaka 2009 akiwa na umri wa miaka 14 Agnes alikwenda Dar es Salaam kutafuta kazi,  akakutana na mtu aliyempa anuani ya hospitali ya CCBRT, anwani iliyobadili maisha ya Agnes daima kwani muda mfupi baadaye aliweza kufanyiwa upasuaji na mabadiliko ni makubwa hakuweza kuficha furaha yake

“Nina furaha sana jinsi ninavyoonekana sasa, nidhani kama nitaogopa tena na nitamatarajio ya mustakhbali wangu kwa sababu Hakuna wa kunicheka tena. Ndoto zangu ni kwenda shule na kupata elimu kama kaka zangu na dada zangu labda siku moja nitaanzisha biashara ya kuchuuza sokoni, jambo ambalo ningeogopa sana kulifikia siku za nyuma.”

Furaha ya Agnes ni tone tu la maji baharini kutokana na kazi kubwa ya kubadili maisha ya watoto na hata watu wazima inayofanywa na CCBRT, kituo cha kijamii kinachotoa huduma ya afya na upasuaji kwa watu wenye ulemavu, hivi sasa kinafanya kazi kwa karibu na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo UNDP.

Watu husafiri kutoka Tanzania nzima kufika kituoni hapo kufanyiwa upasuaji wa aina mbalimbali ikiwemo midomo sungura, ulemavu wa kutoona, fistula  na ulemavu wa viungo.  Kituo hicho kilianzishwa mwaka 1994 na hivi sasa ndio kituo kikubwa zaidi kinachotoa huduma kwa wenye ulemavu Tanzania.

Kila mwaka watu 120,000 wenye ulemavu watoto na watu wazima na wanaowahudumia hubadili afya zao kutokana na huduma za kituo hicho.

Na kwa kupitia uelimishaji, mafunzo na huduma CCBRT inawawezesha watu wenye ulemavu na familia zao kuboresha maisha yao kwa kuwahakikishia fursa ya huduma za afya na matibabu ya kuwarejesha katika hali ya kawaida.