Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amani na uondoaji wa nyuklia ndio iwe shabaha -Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, akizungumza na waandishi habari katika makao makuu ya umoja huo mjini New York
UN Photo/Manuel Elías
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, akizungumza na waandishi habari katika makao makuu ya umoja huo mjini New York

Amani na uondoaji wa nyuklia ndio iwe shabaha -Guterres

Amani na Usalama

Nawapongeza viongozi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK, na Marekani kwa kufuata suluhu ya kidiplomasia kumaliza mvutano wa kinyuklia.

Pongezi hizo zimetolewa  leo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, akizungumza na waandishi habari katika makao makuu ya umoja huo mjini New York Marekani kabla ya viongozi wa mataifa hayo mawili kukutana kwa mara ya kwanza nchini Singapore.

Amesema hatua hiyo ni habari njema na kwamba ni tukio la kuleta matumaini ya amani na usalama duniani.

"Ulimwengu  unasubiri kile kitakachotokea nchini Singapore katika muda wa saa chache zijazo.Nawapongeza viongozi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea na Marekani kwa kufuata suluhisho la kidiplomaisa," amesema Katibu Mkuu.

Katibu Mkuu pia  amewashukuru wale wote waliochangia mazingira ambayo yamewezesha hatua hiyo kufikiwa.

Amewageukia viongozi wawili wa Marekani na DPRK ijulikanayo pia kama Korea kaskazini akiongeza kuwa wanataka kuondoa mzunguko hatari ambao ulizusha wasiwasi mwaka jana huku akisema kuwa “amani pamoja na uondoaji wa nyuklia unaothibitika ni lazima vibaki kama lengo kwa pande zote.Kama nilivyowaandikia wote mwezi uliopita njia waliyoishika itahitaji ushirikiano, maafikiano pamoja na lengo moja”.

Bwana Guterres amewakumbusha kuwa njia waliyofuata ina magumu yake yasiyoepukika  kama vile wakati wa kutokukubaliana na pia majadiliano kuwa magumu wakati fulani.

 Amesema kuwa kuna mifumo muhimu ya Umoja wa Mataifa ambayo iko tayari kusaidia mchakato huu kwa njia yoyote ile hata na uthibitishwaji ikiwa itaombwa na wahusika wakuu.

MASUALA YA NYUKLIA

Ameongeza kuwa shirika la kimataifa la nishati ya Atomiki, IAEA linaweza kutoa mwongozo kuhusu vifaa vyote vya nyuklia vya matumizi ya amani pamoja na vile vitakavyotolewa kutoka  katika mpango wa kijeshi.  Amefafanua kuwa “shirika hilo la kudhibiti matumizi ya nyuklia nalo linaweza kutoa mchango wa kuchunguza  majaribio yaliyotangazwa  na Korea kaskazini kuhusiana na vilipuzi vyake vya nyuklia. Baraza la Usalama kila mara limekuwa likikariri ufumbuzi  wa suala hilo kwa amani na kidiplomasia na kuhimiza kazi za ziada ili kupunguza wasiwasi.” 

HALI YA KIBINADAMU

Kando mwa mzozo wa kisiasa unaoendelea huko DPRK, watu wapatao milioni 10.3 wanaendelea kukabiliwa na njaa, ukosefu wa uhakika wa chakula na lishe duni sambamba na ukosefu wa huduma muhimu. Majanga ya asili nayo yanayotokea mara kwa mara ikiwemo ukame na mafuriko vimeongeza kwa kiasi kikubwa mahitaji ya kibinadamu.

Mahitaji hayo ni pamoja na chakula, lishe, afya, maji na huduma za kujisafi.

Ni kwa kuzingatia mazingira hayo, Katibu Mkuu amehimiza kutilia maanani hali ya kibinadamu nchini Korea Kaskazini ambapo Umoja wa Mataifa unatafuta  dola milioni 111 kuweza kutimiza mahitaji ya watu milioni sita wanaohitaji masaada.

Katibu Mkuu ametaka kutumia nafasi hii kuleta matumaini kwa watu wa rasi ya Korea na ulimwengu mzima kwa ujumla.