Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Iceland kidedea kwenye amani duniani, Syria bado hali si shwari

Uharibifu katika mji wa Homs, Mashariki mwa Syria. Syria ni nchi isiyo na amani zaidi duniani
UNICEF/Penttila
Uharibifu katika mji wa Homs, Mashariki mwa Syria. Syria ni nchi isiyo na amani zaidi duniani

Iceland kidedea kwenye amani duniani, Syria bado hali si shwari

Amani na Usalama

Hali ya amani duniani imeendelea kudorora kwa mwaka wa nne mfululizo.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya kuhusu mwelekeo wa amani duniani kwa mwaka 2018, ambapo sababu za kuzidi kuporomoka kwa amani ni pamoja na kuendelea kwa mivutano, majanga, vita na mizozo ya ndani.

Akiwasilisha ripoti hiyo mbele ya waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, Serge Stroobants wa taasisi ya uchumi na amani amesema.

(Sauti ya Serge Stroobants)

“Nchi 71 zimekuwa na amani zaidi, kwenye nchi 92 amani imeporomoka, na hii ndio maana kwa ujumla kuna kudorora kwa amani.”

Bwana Stroobants akaenda mbali zaidi kutaja maeneo hatari zaidi..

(Sauti ya Serge Stroobants)

“Kwa bahati mbaya, Syria imesalia kuwa nchi isiyo na amani zaidi duniani, nchi iliyoporomoka zaidi ni Qatar kutokana na vikwazo vilivyowekewa nchi hiyo, halikadhalika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa sababu ya matatizo.”

Halikadhalika ripoti hiyo imeweka bayana ni kwa jinsi gani mizozo ya ndani katika nchi za Ulaya imeporomosha viwango vya amani katika nchi ambazo awali zilikuwa na utulivu.

Bwana Stroobants ametolea mfano Hispania ambayo amesema imeporomoka na kushika nafasi ya 30 kutoka 20 kati ya nchi 163 kutokana na mizozo ya ndani iliyogubika nchi hiyo.

Nchi ambayo ina amani zaidi imetajwa kuwa ni Iceland ikifuatiwa na New Zealand, Austria, Ureno na Denmark.

Ripoti hiyo ambayo ni tolea la 12, imesema ghasia zimekuwa na athari hasi kwenye uchumi wa nchi ikielezwa kuwa kiwango hicho cha athari kimeongezeka kwa asilimia 16 tangu mwaka 2012.

Nchi 163 zilihusika kwenye utafiti huo ambapo vigezo vilivyotumika ni pamoja na mizozo ya ndani na nje, ulinzi na usalama kwenye jamii na masuala ya kijeshi.

TAGS: Amani, GPI, Syria, DRC