Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Adhabu ya kifo kwa waislamu wanaokana dini Mauritania si sahihi

Watoto nchini Mauritania.(Picha:UM/Jean Pierre Laffont)

Adhabu ya kifo kwa waislamu wanaokana dini Mauritania si sahihi

Haki za binadamu

Mauritania imetakiwa kuangalia upya ibara  ya 306 ya kanuni ya adhabu inayotaka muumini wa dini  ya kiislamu ahukumiwe kifo iwapo atapatikana na hatia ya kumkashifu Mungu au kukana dini.

Wataalamu hao David Kaye, Agnès Callamard, Ahmed Shaheed na Karima Bennoune wamesema hayo leo katika taarifa yao iliyotolewa huko Geneva, Uswisi.

Wamesema kuwa ibara hiyo inataka mtu aliyetenda kosa hilo ahukumiwe adhabu ya kifo bila uwezekano wowote wa kupatiwa msamaha.

Marekebisho hayo yaliyopitishwa tarehe 27 mwezi Aprili mwaka huu, yanabadili ibara ya awali ambamo kwayo mtu aliyepatikana na hatia ya kukashifu Mungu au kukana dini akionyesha majuto ya kufanya kosa hilo aliweza kupunguziwa adhabu ikawa ya kifungo cha jela badala ya kifo.

“Tumesikitishwa sana na hatua hii kwa kuwa wakati sheria za kimataifa zinazuia uharamishaji wa kukana dini au kumkashifu Mungu, Mauritania imeamua kujumuisha adhabu ya kifo kwa wale ambao watatekeleza haki yao ya uhuru wa kujieleza, kuabudu na kuchagua imani  ya dini,” wamesema wataalamu hao.

Wataalam hao wameongeza kuwa mabadiliko haya yanaendelea kubinya zaidi uhuru wa kujieleza nchini humo na kuweka mazingira ya kuchochea ubaguzi, chuki au ghasia dhidi ya binadamu kwa misingi ya dini au Imani.

Wameisihi serikali ya Mauritania isipigie chepuo ibara hiyo ya 306 ya kanuni ya adhabu na badala yake iiangalie upya ili iweze kwenda sambamba na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.