Ajira bora ni chachu ya amani na mnepo:ILO

7 Juni 2018

Ajira bora na zenye hadhi zimetajwa kuwa ni chachu ya kuchagiza amani na mnepo katika jamii . Hayo yamesemwa na shirika la kazi duniani ILO kwenye mkutano wa 107 wa shirika hilo ambao leo umekuwa na kikao maalumu kilichobeba kauli mbiu “umuhimu wa ajira na ajira zenye hadhi kwa ajili ya amani na mnepo”na kujikita zaidi katika kukabiliana na hali halisi mashinani na pia katika ushirika ambao utazaa matunda.

Mkurugenzi mkuu wa ILO Guy Rider amesema kwa nini mkutano huo ni muhimu

(SAUTI YA GUY RYDER)

“Kwa sababu ya mahitaji yaliyo Dhahiri ya maelfu kwa mamilioni ya wanawake na wanaume wanaoishi katika nchi zenye hali tete na zilizoghubikwa na vita na hali ya majanga. Na ombi tunalilisikia kila wakati ni ajira, mlo, kupata uhuru na utu, elimu kwa watoto wao na wale waliotawanywa wanataka kwenda nyumbani kwa usalama. Na wote tuna hisa ya kuhakikisha mani na mnepo kwa sababu vita na migogoro iliyoota mizizi inatuweka sote hatarini, umasikini popote unasababisha hatari ya mafanikio kila mahali.”

Mkutano huo unashughulikia changamoto za amani ya kudumu kwa kutoa fursa kwenye ulimwengu wa ajira hususani kwa vijana. Baadhi ya wajumbe wanaoshiriki mkutano huo wameelezea mawazo yao kuhusu kuanzisha na kutekeleza mpango ya ajira bora kwenye maeneo yenye hali tete, vita na majanga kama vile Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, ambayo Rais wake ni Faustin-Archange Touadéra

(Sauti ya Faustin-Archange Touadéra)

 “Kwa Jamhuri ya Afrika ya Kati, harakati za kusongesha ajira na kuwa na ajira zenye utu kwa ajili ya nchi yetu na kuwezesha mnepo, ni changamoto ya kila siku. Nimekuja hapa kuwaelezea azma yetu ya kukabiliana na vikwazo katika mchakato wetu wa amani.  Nimekuja pia kuwapatia dira yetu ya kuboresha mazingira ya kazi nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo katu hayaachi kukwamisha uwezo wake wa mnepo. “

 Touadéra amesema anatambua ajira bora ni silaha muhimu

(Faustin-Archange Touadéra)

 “Katika hali ya kawaida, na kwa nyakati zote, ajira ni jambo la msingi kwa uwepo wa jamii. Ajira inabeba vigezo muhimu kwa ajili ya amani ya kudumu. Ufukara ukichochewa na ukosefu wa taarifa, na ukosefu wa ajira huchangia  uwepo wa changamoto kubwa za kukabiliana nazo.”

Mkutano huo ulioanza Juni 5 umewaleta pamoja mjini Geneva Uswis, wadau mbalimbali wa masuala ya ajira , wakiwemo viongozi wa dunia, mashirika ya kimataifa, asasi za kiraia, wataalamu , watunga será, na mashirika ya kibinadamu .Umeandaliwa na shirika la kazi la Umoja wa Mataifa ILO na utakunja jamvi Juni 15.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter