Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kazi shawish hata wanawake tunaiweza: Alya

Mkimbizi mkongwe wa Syria. Ikiwa yuko katika makazi ya Bekka Lebanon matatizo yake yanamulikwa na "Shawish".
UNIFEED
Mkimbizi mkongwe wa Syria. Ikiwa yuko katika makazi ya Bekka Lebanon matatizo yake yanamulikwa na "Shawish".

Kazi shawish hata wanawake tunaiweza: Alya

Wahamiaji na Wakimbizi

Kuwa “shawish nchini Lebanon heshima kubwa na ni lazima uwe na kipawa fulani cha kuongoza na kuweza kubadili mtazamo wa watu, na mara nyingi viatu hivyo huvaliwa na wanaume ambao hutoa maamuzi na pia kusimamia makazi ya wakimbizi. Lakini mwanamke wa miaka 50 amejitoa kimasomaso na kuvaa viatu hivyo kwenye makazi ya wakimbizi wa Syria yaliyoko kwenye Bonde la Bekka Lebanon.Siraj Kalyango anasimulia hadithi ya mwanamke huyo

Huyu ni Alya , mwanamke  mwenye umri wa miaka 50, akiwa kwenye makazi ya wakimbizi ya Bekka kazini kama “shawish” anawahoji wanaume wakimbizi akiwa amevalia shungi kichwani, lakini sio lile  lililozoweleka kwa wanawake, bali ni lile ambaokwa  kawaida huvaliwa na wanaume wa kiarabu wenye mamlaka. Anaeleza sababu ya kuvaa shugi hilo lijulikanalo kama “Shawish”

(SAUTI YA ALYA)

“Wakimbizi wote walitaka mie niwe shawish. Walisema ninaweza kuongoza makazi hayo pamoja na kuhudhuria mikutano.”

Alya sasa ni kiongozi na Shawish. Shawish  ni neno la kiarabu linalotumiwa Lebanon kumuita mwanamme anaesimamia wafanyakazi wa kigeni katika shamba au ujenzi. Lakini tangu kuzuka kwa mgogoro nchini Syria na wakimbizi kuanza kumiminika Lebanon, neno hilo sasa limepata maana mpya kama anavyofafanua Alya

(SAUTI YA ALYA)

“ Ikitokea suala lolote au mfarakano naingilia kati na kutatua shida zao  na kuwapatanisha watu hao na hatimae  kuwaleta pamoja.”

 

Shawish  ni neno la kiarabu linalotumiwa Lebanon kumuita mwanamme anaesimamia wafanyakazi wa kigeni katika shamba au ujenzi

Alya amezaliwa na kulelewa katika jamii ya mfumo dume lakini malezi na mafunzo toka kwa baba yake ndiyo yaliyompa ujasiri yeyé na dada zake

(SAUTI YA ALYA)

“Alituambia wasichana muwe wakakamavu, na mtetee haki zenu. Na hata mwanamme akiwa anawagombanisha msinyamaze kimya jiteteeni.”

Katika makazi ya wakimbizi “shawish” huwa ni mkimbizi anaefanya kazi ya kusimamia wenzie na ni mtu mwenye kutoa maamuzi. Mtu huyo ndiye kiungo kati ya wakimbizi na mashirika mbalimbali yawe ya kitaifa au kimataifa hususan ya misaada kama vile ya Umoja wa Mataifa likiwemo la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Majukumu mengine anayohusika nayo ni  kusajili makazi  ya wakimbizi kwa  mashirika ya misaada,anasimamia usambazaji wa misaada hiyo na kutatua migogoro baina ya wakimbizi.

 

Mtoto wa miaka mitano akiishi na Bibi yake katika nyumba iliyobomolewa Syria. Angekuwa Bekka Lebanon shida zake zingetatuliwa na "Shawish".
Picha ya UNICEF/UN066023/Almohibany
Mtoto wa miaka mitano akiishi na Bibi yake katika nyumba iliyobomolewa Syria. Angekuwa Bekka Lebanon shida zake zingetatuliwa na "Shawish".

 

Na je wakimbizi anaowahudumia Alya wanamuonaje?

(SAUTI YA AIDA)

“Alya ni mtu mtulivu na mvumilivu. Kazi ya Ushawish si mchezo inasababisha msongo wa mawazo.”

Alya halipwi chochote kutokana na kazi ya Ushawish, lakini anasema huhisi furaha kusaidia watu wengine na kazi hiyo inampa faraja na fahari kubwa .