Tuna hofu kubwa baada ya wahamiaji 100 kufa maji Tunisia:IOM

5 Juni 2018

Wahamiaji takriban 100 wamekufa maji, 68 kunusurika na wengine hawajulikani waliko baada ya boti yao kuzama mwambao wa Kerkennah-Sfax nchini Tunisia mwishoni mwa wiki.

Kwa mujibu wa shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa IOM hizi ni ripoti za awali zilizopatikana Juni 3 ambazo zinasema wahamiaji 180 walianza safari isiyo na uhakika kuelekea Ulaya kwa kutumia boti iliyokuwa imefurika na ndio mkasa ulipowasibu.

Lorena Lando mkuu wa IOM Tunisia amesema miongoni mwa maiti 60 zilizopelekwa idara ya uchunguzi ya hospitali ya Habib Bourguiba mjini Sfax Tunisia, zimebainika kuwa 48 ni raia wa Tunisia na 24 kati yao wameshatambuliwa , huku raia 12 ambao sita ni wanawake na sita ni wanaume sio Watunisia na shughuli ya kutambua maiti zilizosalia inaendelea.

Ameongeza kuwa kwa upande wa manusura 68, sitini kati yao ni Watunisia, wawili kutoka Morocco, mmoja kutoka Libya, mmoja kutoka mali, mmoja kutoka Cameroon na raia watatu ni wa Cote D’voire wakiwemo wanawake wawili.

IOM inasema wahamiaji hao wameripotiwa kulipa kati ya Euro 700 na 1000 ili kusafirishwa hadi Ulaya. Shirika hilo limetoa wito wa kuchukua hatua za mazungumzo na ushirikiano ili kuweza kuwalinda wahamiaji licha ya hali yao ya kutokuwa na vibali, na limependekeza kufanyika kampeni zinazolenga hatari dhidi ya wahamiaji na kuchagiza njia mbadala za kisheria zitakazofanya watu kupata taarifa sahihihi kuhusu uhamiaji na kuufanya kuwa ni chaguo na sio lazima.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter