Nchi masikini zapata mkombozi, Benki ya teknolojia:UN
Chombo kipya chenye lengo la kushughulikia changamoto za mataifa maskini duniani kimezinduliwa rasmi hi leo mjini Gebze nchini Uturuki.
Chombo hicho ambacho ni “Benki ya Teknolojia”, kitashughulikia matatizo ya nchi hizo maskini kupitia sayansi, teknolojia pamoja na ubunifu.
Akihutubia wakati wa uzinduzi wa chombo hicho ,Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bi Amina Mohammed, amesema uzinduzi huo ni wa muhimu katika kusaidia mataifa yaliyo na maendeleo duni -LDCs kuweza kujiendeleza kwa kutumia faida za sayansi, teknolojia na ubunifu. Akisisitiza umuhimu wa chombo hicho wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini New York hii leo, kwa kumnukuu Bi Mohammed, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema
(SAUTI YA STEPHANE DUJARRIC)
“Kuundwa kwa benki ya teknolijia kunadhihirisha azma ya ulimwengu kuhakikisha kwamba mataifa yote yanaweza kutumia vifaa vya hali ya juu ili kufanikisha malengo yote endelevu”
Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, lilipitisha kuundwa kwa Benki ya Teknolojia , ili ibebe jukumu la kuimarisha uwezo wa maarifa au ufahamu wa mataifa 47 yenye maendeleo duni, kwa minajili kuchochea maendeleo na ubunifu wa mifumo yake ya teknolojia ya kitaifa na kikanda ili kuweza kuvutia teknolojia ya nje kwa lengo la kukuza uwezo wake wa ndani wa utafiti na ubunifu.
Bi Mohammed amesema uzinduzi wa leo ni tukio muhimu la kihistoria katika kusaidia mataifa yenye maendeleo duni kutumia faida za sayansi, teknolojia na ubunifu, ili kutilia mkazo ufikiaji wa ajenda ya maendeleo yam waka 2030 ambayo inataka kuhakikisha “hakuna atakaeachwa nyuma” kwani huo ndio ufunguo.
Ameongeza kuwa chombo hiki kinatarajiwa kuboresha matumizi ya kisayansi kwa mataifa maskini kuweza kupata uchumi ambao unaegemea maarifa.