Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Choo 1 kwa watu 200 nchini Marekani, ajabu na kweli

 Philip Alston, Mwakilishi Maalum kuhusu umaskini uliokithiri na haki za binadamu.
Picha ya UN /Evan Schneider
Philip Alston, Mwakilishi Maalum kuhusu umaskini uliokithiri na haki za binadamu.

Choo 1 kwa watu 200 nchini Marekani, ajabu na kweli

Haki za binadamu

Huwezi kuamini lakini nchini Marekani kuwa maskini ni jambo ambalo mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa anasema kunachochewa na dharau na sera za kikatili.

Nchini Marekani watu milioni 40 wanaishi katika umaskini ingawa nchi hiyo inaongoza kwa kuwa tajiri zaidi duniani.

Mtaalamu  huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu umaskini uliokithiri na haki za binadamu Philip Alston amesema hayo katika ripoti yake mpya baada ya kufanya ziara kwenye maeneo manne nchini humo.

Maeneo hayo ni California, Alabama, Georgia, Virginia Magharibi na Washington D.C ambako alishuhudia vitendo vya kikatili na dharau dhidi ya maskini vikiendana na sera za kikatili dhidi ya maskini.

“Utawala wa Trump umekuja na sitisho kubwa la muda la kodi dhidi ya kampuni na matajiri huku ukipigia debe mbinu za kukata mfumo wa ustawi wa jamii,” amesema Alston.

Amesema mfumo huo unaonekana kuwafungia wa maskini kwa kuwa unaongeza tofauti kubwa kati ya maskini na matajiri na kutumbukiza mamilioni ya wamarekani wafanyakazi na wasio na uwezo wa kufanya kazi kwenye ufukara.

“Kinachoonekana zaidi ni dharau kwa maskini na wakati mwingine chuki dhidi ya maskini ambako kumesheheni fikra za mshindi achukua vyote,” amesema mtaalamu huyo huru ambaye ripoti yake ataiwasilisha mbele ya Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa tareha 21 mwezi huu.

Mtu asiye na makazi akiwa ameketi kwenye ngazi za duka moja eneo la Manhattan, jijini New York, nchini Marekani
UN/Pernaca Sudhakaran
Mtu asiye na makazi akiwa ameketi kwenye ngazi za duka moja eneo la Manhattan, jijini New York, nchini Marekani

Ushahidi wa dharau na chuki dhidi ya maskini iko dhahiri akitolea mfano huko Skid Row huko Los Angeles jimboni California ambako watu 14,000 wasio na makazi walikamatwa mwaka 2016 kwa kujisaidia haja ndogo kwenye eneo la umma.

Bwana Alston amesema watu hao wasio na makazi hawakuwa na la kufanya kwa kuwa katika mji huo hakuna vyoo vya umma na choo kimoja kinahudumia watu 200.

Amesema uwiano huo ni wa chini zaidi akisema hata haufikii kiwango cha kwenye kambi za wakimbizi wa Syria zinazoendeshwa na Umoja wa Mataifa.

Halikadhalika amegusia mfumo wa sheria wa Marekani akisema uko kwa ajli ya kukusanya mapato kwa ajili ya majimbo na si kusaidia maskini.

Mfano mwingine ametoa ni kuhusu wanasiasa ambao amesema baadhi ya aliozungumza nao wana fikra ya kwamba wa maskini ni matapeli na wanaishi kwa kutegemea mfumo wa ustawi wa jamii pekee.

“Marekani inaongoza kwa nchi za magharibi kwa kuwa na pengo kubwa la ukosefu wa usawa kwenye kipato na pia idadi ndogo ya watu wanaojitokeza kupiga kura miongoni mwa nchi zilizoendelea,” amesema Alston akihitimisha kuwa matokeo yake demokrasia Marekani inakabiliwa na tishio kubwa kwa sababu ya ufukara na sera zinazozidi kudidimiza demokrasia.