Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baiskeli yatambuliwa katika kuchagiza SDGs

Mwanamke anasafiri akitumia baiskeli barani Afrika. Picha: UNEP

Baiskeli yatambuliwa katika kuchagiza SDGs

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kwa mara ya kwanza siku ya baiskeli imeadhimishwa hii leo na lengo ni kuchagiza maendeleo endelevu.

Je wafahamu kuwa baiskeli ina siku yake maalum ya kuadhimishwa duniani?

Siku hiyo ni leo Juni 3 ikiwa ni maadhimisho ya kwanza yaliyoridhiwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UN.

UN inataja sababu lukuki za kusherehekea baiskeli ambazo ni pamoja na kwamba baiskeli ni rahisi kuitumia, inanunulika, ni chombo rafiki cha usafiri kwa mazingira.

Kama hiyo haitoshi, UN inasema "baiskeli inajenga urafiki kati ya mtumiaji na mazingira yanamzunguka kwa kuwa anaweza kufahamu eneo analoishi."

Mvulana akiendesha baiskeli huko wilayani Gatsibo nchini Rwanda kwenda kuteka maji kwenye mradi wa maji uliofadhiliwa na serikali.
World Bank/A'Melody Lee
Mvulana akiendesha baiskeli huko wilayani Gatsibo nchini Rwanda kwenda kuteka maji kwenye mradi wa maji uliofadhiliwa na serikali.

Zaidi ya yote, UN inasema kuwa baiskeli ni ishara ya chombo endelevu cha usafiri na kinatumika pia kwa michezo na kuboresha afya ya mtumiaji.

Kwa mantiki hiyo kupitia siku hii, nchi wanachama zinachagizwa kuweka umuhimu baiskeli katika sera zao za maendeleo.

Mathalani kuhakikisha usalama kwa watumiaji wa baiskeli barabarani kwa kuweka miundombinu ya kuwawezesha kuendesha baiskeli kwa usalama zaidi.

UN pia inahamasisha wadau "kuchagiza matumizi ya baiskeli kama njia ya kusongesha maendeleo endelevu ikiwemo ya afya kwa kuwa kuendesha baiskeli ni mazoezi yanayoweza kuepusha magonjwa yasiyo ya kuambukiza yatokanayo na sababu mbalimbali ikiwemo utipwatipwa."