Mapigano Afghanistan yaengua mamilioni ya watoto shuleni Afghanistan

2 Juni 2018

Mustakhbali wa watoto Afghanistan mashakani kutokana na mapigano

Takribani nusu ya watoto wenye umri wa kati ya miaka 7 hadi 17 nchini Afghanistan hawako shuleni.

Hii ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF iliyotolewa leo ikiangazia watoto wasio shuleni ikijikita zaidi nchini Afghanistan.

Sababu kuu zinatajwa ni mzozo unaoendelea nchini humo sambamba na umaskini na ubaguzi dhidi ya watoto wa kike.

Watoto hao milioni 3.7 wasio shuleni ni kiwango cha cha juu zaidi kuwahi kufikiwa nchini Afghanistan tangu mwaka 2002, imesema ripoti hiyo.

Asilimia 60 ya watoto hao ni watoto wa kike, hali ambayo ripoti hiyo imesema inawaweka katika hali mbaya zaidi kwa kuzingatia ubaguzi na ukatili mwingine wanaokabiliana nao kutokana na jinsia yao ikiwemo ndoa katika umri mdogo.

Majimbo ambamo kwayo watoto wa kike wana hali mbaya zaidi kielimu ni Kandahar, Helmand, Wardak, Paktika, Zabul na Uruzgan.

Akizungumzia ripoti hiyo, mwakilishi wa UNICEF nchini Afghanistan, Adele Khodr amesema kuendelea kuchukua hatua za kawaida hakutaleta manufaa yoyote iwapo jamii ya kimataifa inataka kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya elimu.

UNICEF/Rezayee
Takribani familia 200 zinaishi katika kijiji hiki nchini Afhganistan ambako watoto wa kike walioozwa au ambao umri wao ni mkubwa wanasoma katika kituo cha mafunzo cha UNICEF.

“Pindi watoto wanapokuwa hawapo shuleni, wako katika hatari zaidi ya kukumbwa na unyanyasaji, ukatili na kutumikishwa,” amesema mwakilishi huyo wa UNICEF.

Hata hivyo ripoti imesema kando mwa mwelekeo huo unaokatisha tamaa bado kuna matumaini kwa kuwa, “viwango vya utoro shuleni ni vya chini kwa wasichana na wavulana, changamoto ni kuwawezesha watoto kuanza shule,” imesema ripoti hiyo.

Mwakilishi wa UNICEF amepongeza serikali ya Afghanistan kwa kupatia kipaumbele elimu na kutangaza kuwa mwaka 2018 ni mwaka wa elimu.

Mtoto Feizia mwenye umri wa miaka 12 ni mkimbizi wa ndani nchini Afghanistan. Nduguze watatu waliuawa huku mama yake akichomwa na kisu ndani ya kambi yao. Hivi sasa anaishi kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani huko Afghanistan. (picha:UNICEF-videocapture)
Mtoto Feizia mwenye umri wa miaka 12 ni mkimbizi wa ndani nchini Afghanistan. Nduguze watatu waliuawa huku mama yake akichomwa na kisu ndani ya kambi yao. Hivi sasa anaishi kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani huko Afghanistan. (picha:UNICEF-videocapture)

Sasa ni wakati wa kurejelea ahadi yetu ya kuwapatia watoto wa kike na wa kiume fursa mujarab za kujifunza ambazo wanahitaji ili kusongesha maisha yao na kuwa na mchango stahili katika jamii zao,” amesema mwakilishi huyo.

UNICEF imetaka kuwepo kwa fursa za mapema kwa mtoto kuanza kujifunza kuanzia ngazi ya jamii, kwa kuwa na madarasa ya karibu ili kuepusha hatari anayokumbana nayo mtoto hususan wa kike anapokwenda shuleni.

Halikadhalika kuondokana na mila potofu kama vile ndoza za umri mdogo na familia ziwe na uwezo wa kupaza sauti kuhusu elimu ya mtoto ikielezwa kuwa elimu ya mtoto ni zaidi ya kuwa darasani.
 

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter