Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakati msimu wa monsoon unabisha hodi Bangladesh, IOM yagawa msaada muhimu

Mkimbizi kutoka Rohingya katika kambi ya Cox's Bazar akijiandaa na pepo za monsoon
Picha WFP/Saikat Mojumder
Mkimbizi kutoka Rohingya katika kambi ya Cox's Bazar akijiandaa na pepo za monsoon

Wakati msimu wa monsoon unabisha hodi Bangladesh, IOM yagawa msaada muhimu

Tabianchi na mazingira

Wakati wakimbizi wa Ronhingya kwenye kambi za Cox’s Bazar  na jamii zinazowahifadhinchini Bangladesh wakijiweka tayari kwa msimu wa monsoon unaoambatana na upepo mkali na mvua kubwa, shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa IOM, kwa kushirikiana na serikali ya Bangladesh wapo mstari wa mbele kuhakikisha watu hao wanapata  msaada wa hali na mali ili kukabiliana na janga hilo

Misaada hiyo ni pamoja na redio, vipaza sauti, mahitaji ya dharura, dawa na chakulamsaada uliotolewa kwa zaidi ya wakimbizi 500 ambao wamepewa mafunzo ya dharura katika kambi ya Kutapolong na  wengine zaidi ya 1000 katika kambi ya Cox’s Bazar.

Kuna makadirio ya wakimbizi milioni moja katika kambi ya wakimbizi ya Cox’s Bazar ambao walikimbia mapigano ya kikabila kaskazini mwa Myanmar na zaidi ya laki mbili kati yao wapo katika hatari ya kuathirika na maporomoko ya udongo katika msimu huu wa monsoon.

Vikosi vya usalama vya Bangladesh kwa ushirikiano na chama cha msalaba mwekundu cha Marekani na hilali nyenkundu ya Bangladesh wamekuwa wakiendesha mafunzo ya kujiandaa na janga la monsoon tangu mwaka 1972. Na baada ya wimbi kubwa la wakimbizi kuingia nchini humo sasa IOM imeamua kuwajumuisha wakimbizi katika mafunzo hayo ili waweze kujiandaa  vyema na msimu huo wa monsoon .

Rafael Abis mratibu wa IOM katika kambi za wakimbizi huko Bangladesh amesema maandalizi kwa wakimbizi wanaojitolea  ni muhimu sana  maana watachukua ujuzi huu na kuusambaza kwa wenzao ili kupunguza hatari kwa waathirika wa pepo za monsoon.

Kwa upande wake Laila ambaye ni mmoja wa wakimbizi waliofanikiwa kupata mafunzo ya dharura, anasema kwa sasa anajiamini na  pia vifaa walivyopewa vitaweza kusaidia kuokoa maisha ya watu.

IOM na mashirika wadau wako tayari kuendelea kutoa msaada kwa wakimbizi wakati huu ambapo wanakabiliwa na hatari ya msimu wa  monsoon .