Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Juhudi dhidi ya matumizi ya plastiki zitumikazo mara moja zapamba moto

Plastiki zitupwazo kiholela nyingine huishia baharini na kuwa tatizo kubwa kwa viumbe vya baharini.
Cyril Villemain/UNEP
Plastiki zitupwazo kiholela nyingine huishia baharini na kuwa tatizo kubwa kwa viumbe vya baharini.

Juhudi dhidi ya matumizi ya plastiki zitumikazo mara moja zapamba moto

Tabianchi na mazingira

Ulimwengu unahitaji ufumbuzi mbadala dhidi ya  matumizi ya vifaa vya plastiki vinavyotumika mara moja na kutupwa.

Kauli hiyo imetolewa leo mjini Nairobi, Kenya na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNE, Erik Solheim, wakati wa uzinduzi wa ripoti mpya inayotathmini uwezekano wa kuachana na plastiki zinazotumika mara moja na kuibuka na njia mbadala.

Bwana Solheim amesema kubadili mtindo wa  kutumia plastiki zinazotupwa punde baada ya kutumiwa hadi vyombo vingine mbadala, ni uwekezaji wa muda mrefu wa mazingira yetu.

Ripoti hii imechapishwa kwa kile ofisi ya mazingira ya Umoja wa Mataifa ilichoita,"juhudi za kuupatia ulimwengu maarifa ya kupunguza utupaji hovyo wa taka za plastiki na taka hizo kuishia baharini,kwenye mito na maziwa."

Ripoti inasema bahari zimezidi kuwa kama jalala la taka za plastiki hatua ambayo ina athari iliyodhihirishwa kijamii, kiuchumi na kimazingira.

Bwana Solheim amesisitiza kuwa vifaa mbadala vina mchango katika kupunguza utegemezi kwa plastiki.

Mmoja wa walioandika ripoti hiyo, Peter Kershaw,amesema inalenga kuihamasisha jamii kujiuliaza kuhusu matumizi ya sasa ya plastiki na kufikiria matumizi mbadala, akitilia mkazo zile bidhaa ambazo zinatengenezwa kwa matumizi ya mara moja.

Mwanasayansi mkuu katika shirika hilo, Jian Liu, amesema, sayansi inaweza kusaidia jamii ya kibiashara kuwa na suluhisho mbadala ambalo haliharibu mazingira.   

“Kuna nafasi kubwa katika nyanja za ajira na biashara katika ubunifu na uendelezaji wa bidhaa mpya za ubunifu ambazo zitachukua pahala pa plastiki za kutumia mara moja tu,” amesema.

Ripoti imekariri baadhi ya vyanzo vya plastiki mbadala kama vile karatasi, pamba, na mbao pamoja na mwani, maganda ya mananasi pamoja na mengine.

Ripoti imezinduliwa kuendana na siku ya mazingira duniani ya mwaka 2018 inayoadhimshwa kila tarehe ya 5 Juni.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni 'Shinda uchafuzi wa plastiki".