Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vyama vya ushirika ni mkombozi kwa mkulima maskini- FAO

Mkulima katika shamba lake lililoshambuliwa na viwavi jeshi huko Namibia
FAO/Rachael Nandalenga
Mkulima katika shamba lake lililoshambuliwa na viwavi jeshi huko Namibia

Vyama vya ushirika ni mkombozi kwa mkulima maskini- FAO

Ukuaji wa Kiuchumi

Wakati kilimo cha kibiashara kinaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kuchagiza maendeleo ya kiuchumi barani Afrika, Umoja wa Mataifa unasema hilo linawezekana zaidi iwapo mkulima wa kijijni naye atajengewa uwezo kupitia vyama vya ushirika.

Mkurugenzi Mkuuwa shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO,  José Graziano da Silva amesema hayo leo huko Utretch nchini Uholanzi wakati wa mkutano wa tatu wa kimataifa kuhusu chakula kwanza, kipaumbele kikipatiwa ujasiriamali kwenye kilimo au kilimo biashara.

Amesema sera bora na ubia unatakiwa barani Afrika lakini hiyo pekee haitoshi kwani lazima kuimarisha vyama vya ushirika ambavyo ndio mkombozi wa mkulima mashinani.

Bwana da Silva amesema bila hivyo, watakaonufaika na kilimo cha kibiashara watakuwa wakulima wakubwa ambao wanashikilia mchakato mzima wa chakula kuanzia kilimo mashambani hadi sokoni.

Yaelezwa kuwa kilimo barani Afrika kinatarajiwa kuchangia dola trilioni moja ifikapo mwaka 2030.

Kwa mantiki hiyo FAO imesema ili wakuliwa wadogo wasibakie nyuma katika kunufaika na fursa hiyo, vyama vya ushirika ambavyo kwavyo mkulima anaweza kupata sauti, ni lazima viangaziwe na kujengewa uwezo ili uzalishaji uwe wa kisasa na uendane na mahitaji ya soko.

"Vyama vya ushirika na vinginevyo ndio njia pekee ya kuwapatia wakulima wadogo usaidizi wa kiufundi, kuwajengea uwezo, kuwapatia msaada wa fedha na pia teknolojia za kisasa,” amesema Bwana da Silva akisema hatua hizo ziende sambamba na kuboresha huduma za kijamii kama vile afya na elimu na teknolojia ya mawasiliano.

“Hii itasaidia kuunganisha wazalishaji, wachakataji wa mazao na pia wahusika wengine katika mlolongo mzima wa kutoa chakula shambani hadi mezani,” amehitimisha Bwana da Silva.

Ni kwa mantiki hiyo FAO na taasisi ya Rabbobank wameingia ubia ili kusaidia wakulima wadogo na vyama vya ushirika kwenye nchi zinazoendelea waweze kujitegemea kiuchumi.

Tayari nchini Tanzania, wabia hao wamesaia wakulima wa mpunga na mihogo kuwa na mbinu bunifu za umwagiliaji na uhifadhi wa mazao.

TAGS: FAO, Rabbobank, Tanzania, vyama vya ushirika