Wakimbizi walio taabani Jordan waomba msaada usikatwe

1 Juni 2018

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR linahitaji msaada wa haraka wa dola milioni 116 ili kuendeleza mpango wa kusaidia wakimbizi wa Syria wasiojiweza nchini Jordan.

UNHCR inasema fedha hizo zisipopatikana, italazimika kukata msaada wa fedha kwa wakimbizi wa Syria walioko Jordan ikiwemo walio taabani.

Mjini Amman, Jordan, ndani ya moja ya chumba cha wakimbizi, anaonekana Saif mkimbizi huyu kutoka Syria akijikongoja, usoni akionekana na maumivu makali.

Anasema mateso, kupigwa, udhalilishaji, njaa, baridi na hofu ni mambo yaliyomkumba akiwa mfungwa kwa miaka miwili kwenye gereza la Dera’a huko Syria.

Sasa hawezi kutembea. Mama yake mzazi ambaye wanaishi naye hapa, naye anaugua saratani ya koo.

Wanaishi Jordan tangu mwaka 2014, ambapo hali haikuwa shwari kama anavyoeleza Saif.

(Sauti ya Saif)

“Hali ya kifedha ilikuwa mbaya sana. Fikiria baadhi yetu tuliachana na  mambo ya dawa kwa sababu tulikuwa hatuwezi kulipia.”

Nchini Jordan, Saif alipata tiba ya majeraha na mama yake tiba ya saratani, lakini hawakuwa na uwezo wa kununua dawa zilizohitajika.

UNHCR
Ramani ikionyesha idadi ya raia wake walioko ukimbizini nje ya nchi

 

Mwaka 2016, UNHCR ilianza kuwapatia fedha za matibabu. Saif sasa akiwa kitandani anachambua vyeti vyake vya matibabu.

Kwa msaada huo, aliweza kumudu gharama za tiba na mazoezi ya viungo na hata kupatiwa mkongojo wa kumwezesha kutembea.

(Sauti ya Saif)

“ Nilipoanza kupokea msaada wa fedha, hali yangu ilibadilika. Niliweza kununua dawa na kumsaidia mama kwa kumlipia kodi ya nyumba. Hali ilibadilika na nilijihisi sawa kisaikolojia na kimwili.”

 Hata hivyo hivi sasa kuna hofu ya kwamba fedha hizo ambazo ni dola 112 kwa mwezi zinaweza kuondolewa na hivyo Saif anasema…

(Sauti ya Saif)

“Ikiwa watakata msaada, hii ina maana mimi na mama yangu itatubidi turejee Syria. Basi hata kama itabidi kufia huko, katu hatutakuwa ombaomba.”

Kwa sasa UNHCR inahaha kupata msaada ili kuendeleza mpango huo, la sivyo utakoma ifikapo julai mosi mwaka huu.

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter