Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN sasa kuwa na mashiko mashinani- Guterres

Vijana nchini Somalia wanashirikiana kuendeleza malengo ya maendeleo endelevu. Picha: AMISOM

UN sasa kuwa na mashiko mashinani- Guterres

Masuala ya UM

Baada ya mashauriano ya muda mrefu, hatimaye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeridhia mapendekezo ya marekebisho ya mfumo wa maendeleo wa chombo hicho chenye wanachama 193. Marekebisho hayo yanalenga kusogeza zaidi UN kwa wananchi wa kawaida ili hatimaye maendeleo yawe dhahiri ya watu na si vitu.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UN, kwa kauli moja limepitisha azimio la kubadilisha mfumo wa utekelezaji wa shughuli za maendeleo za umoja huo.

Muundo mpya uliopendekezwa na Katibu Mkuu wa UN,  unalenga kuwezesha chombo hicho kutekeleza kwa vitendo malengo yake ya maendeleo endelevu, SDGs na hivyo kuhakikisha chombo hicho kinalenga maendeleo ya watu na hakuna anayeachwa nyuma.

Kuna hatua 7 zilizopendekezwa na Katibu Mkuu kupitia azimio hilo ambazo ni pamoja na kuwepo kwa mratibu mkazi atakayewajibika zaidi kwenye mahitaji ya nchi husika katika kutekeleza ajenda 2030 kwa kuzingatia uzoefu, stadi na ufahamu uliopo ndani ya Umoja wa Mataifa.  Halikadhalika mfumo wa ufadhili na uchangiaji wa fedha unaohakikisha upatikanaji wa uhakika wa fedha.

Maendeleo vijijini yatajwa kama wajibu wa kimaadili.(Picha:IFAD/Guy Stubbs)

MFUMO MPYA WA MAENDELEO WA UN

Akizungumza baada ya kura hiyo, jijini New York, Marekani, Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres ameshukuru nchi wanachama kwa kuridhia mpango huo akisema azimio lililopitishwa hii leo linafungua mlango wa marekebisho ya hali ya juu na ya kina ya mfumo wa maendeleo wa Umoja wa Mataifa kuwahi kufanyika katika miongo kadhaa.

Na zaidi ya yote amesema linaweka misingi ya kuweka upya maendeleo endelevu kwenye kitovu cha Umoja wa Mataifa. Mathalani Bwana Guterres amesema..

 (Sauti ya Antonio Guterres)

“Mwisho wa siku, marekebisho haya yanaweka mfumo ambao utaleta tofauti  halisi katika maisha ya watu. Mmekuwa dhahiri katika mamlaka yetu kuanzisha kizazi kipya cha timu za UN kwenye nchi na kuimarisha uwekezaji kwa watu, sayari, amani na ustawi. Umiliki wa kitaifa wa mpango huu na kuangazia kwa kina uwajibikaji na matokeo, vitakuwa ni mwongozo kwa kila hatua.”   

Marekebisho mwisho wa siku ni kuweka mfumo wa kuleta tofauti bora katika maisha ya watu.

 

Mapema Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed ambaye aliongoza mchakato wa mfumo huo mpya, amehojiwa na Idhaa ya umoja huo na kuelezea hasa sababu ya muundo huo. 

(Sauti ya Amina J. Mohammed)

“Ni kwamba tumepata mpango mpya tuliokubaliana mwaka 2015, yaani ajenda ya 2030 yenye malengo 17 inayojumuisha pia mabadiliko ya tabianchi. Kwa hiyo ni chepuo kubwa katika kile unachohitaji kwenye mfumo wa UN ili uweze kushughulikia ipasavyo pale malengo ya milenia, MDGs yalipokomea.”

Bi. Mohammed amesema ni kwa mantiki hiyo UN inahitaji kujipanga upya na kuwa na seti nzima ya stadi. “Tunahitaji kuhakikisha watendaji katika ngazi ya nchi wana uwezo wa kusaidia mataifa husika na watu wafikie ndoto zao ambazo tumejumuisha kwenye ajenda yetu,” amesema Naibu Katibu Mkuu huyo wa UN.

Alipoulizwa ni kwa jinsi gani mfumo huo mpya utaongeza ufanisi, Bi. Mohammed amesema, “bila shaka kwani ufanisi wa UN utakuwa wa kipekee kwa sababu tutakuwa na kiongozi ambaye yuko huru na haegemei upande wowote kwenye mfumo wetu lakini katika ngazi ya nchi, na huyo ataweza kuweka timu yetu pamoja.”

Bi. Mohammed akaenda mbali kutofautisha mfumo mpya na wa zamani akifananisha na kiongozi wa kwaya ambaye anaimbisha kwaya huko mkono wa kushoto haufahamu mkono wa kulia unafanya nini.

Umoja wa kimataifa kuwafikia vijana katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania kuwaelimisha kuhusu malengo ya maendeleo endelevu SDG's. Picha: Photo - Zainul Mzige

UCHANGIAJI WA MFUMO MPYA

Naibu Katibu Mkuu akagusia pia suala la ufadhili akisema kuwa kinachoonekana sana UN inatumia fedha kidogo sana kwenye masuala ya maendeleo.

Mfumo mpya kupitia waratibu wakazi wanaoripoti kwa Katibu Mkuu na serikali ya nchi husika unataka bajeti kwa afisa huyo itokea kwa nchi wanachama na UN.

“Kile tunachotaka ni nchi wanachama ziongeze fedha zaidi kwenye miradi ya umma na pia zichagize sekta binafsi. Mfumo mpya hauwezi kutekelezwa na UN peke yake au nchi wanachama. Unahitaji ubia ambao ndio maana lengo namba 17 la malengo endelevu ni muhimu.”

NCHI WANACHAMA ZIKAUNGA MKONO

Kabla ya kupiga kura, wawakilishi wa kudumu wa Algeria, Denmark, Marekani na India walizungumza wakipigia chepuo mfumo huo mpya.

Kwa ujumla walikaribisha wakisema litachagiza maendeleo ya wananchi na kuhakikisha kuwa mchango wa fedha kutoka kwa nchi wanachama unakuwa na manufaa kwa wananchi.

Ethiopia ikizungumza kwa niaba ya Afrika imesema azimio limekuja wakati muafaka katika kufanikinisha SDGs na ni hatua ya kwanza katika marekebisho ya Umoja wa Mataifa, ambayo yatahitaji mashauriano zaidi.

Hata hivyo imesema “tunataka kuona uwepo wa UN kwenye nchi wanachama wenye ufanisi zaidi, na hatutaki kuwa nyuma katika utekelezaji wa ajenda ya maendeleo endelevu.”

Hatua ya leo inafuatia mjadala na mashauriano ya muda mrefu kati ya UN na nchi wanachama wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Bi. Mohammed.

Bwana Guterres amewahakikishia wajumbe kuwa ataanza mchakato wa kuandaa muundo uliopitishwa huku akiahidi mshikamano kutoka kwa nchi wanachama ili uanze kutekelezwa tarehe mosi Januari mwakani.

TAGS: UNDAS, Antonio Guterres, Amina J. Mohammed, Umoja wa Mataifa