Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahudumu wa ndege nao kuangazia wasafirishaji haramu wa binadamu

Usafirishaji haramu.(Picha:UNODC)

Wahudumu wa ndege nao kuangazia wasafirishaji haramu wa binadamu

Haki za binadamu

Umoja wa Mataifa umechukua hatua zaidi ili kuepusha usafirishaji haramu wa binadamu.

Hatua za hivi karibuni zaidi ni uzinduzi wa mwongozo wa mafunzo kwa wahudumu wa ndege na wafanyakazi wa viwanja vya ndege.

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa na shirika la usafiri wa anga, ICAO wamezindua mwongozo huo wakisema kuwani hatua muhimu ili kudhibiti  vitendo hivyo vinavyambatana na  ukatili wa wahanga wakati wanaposafirishwa kinyume na matakwa yao.

Naibu Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Kate Gilmore amesema katika biashara haramu ya sasa ya binadamu, usafirishaji ndio msingi mkuu. “Idadi kubwa ya wasafirishaji haramu wanahaha kuepuka kubainiwa na mamlaka, na hivyo wanatumia mbinu za kisiri za usafirishaji huku wengine wakiwa jasiri na kutumia usafiri wa umma kuanzia teksi, mabasi ya umma hadi ndege za abiria,,” amesma Bi. Gilmore.

Kwa mantiki hiyo amesema matumizi ya njia bora na sahihi  ni muhimu ili kuepuka mbinu hizo za kijanja na hivyo ni wajibu wa Umoja wa Mataifa kuvunja mpango huo.

Naye Katibu Mkuu wa ICAO Dkt. Fang Liu amesema ni wajibu wa kila nchi mwanachama wa ICAO kuwajibisha mashirika yao ya ndege kutumia mwongozo huo wa mafunzo ili kupunguza na hatimaye kuondokana na usafirishaji haramu wa binadamu kwa njia ya anga.


Wakati wa mkutano huo huko Geneva, Uswisi, washiriki walisikia simulizi kutoka kwa mhudumu wa ndege Donna Hubbard ambaye alibakwa na genge la wasafirishaji haramu ili aweze kuokoa familia yake ambayo walikuwa wanaishikilia.

Hubbard amesihi mashirika ya ndege kuajiri wahanga wa matukio ya usafirishaji haramu, hatua ambayo siyo tu itawaepusha na janga hilo bali pia itawapatia utaalamu wa kubaini wasafirishaji haramu.

Shirika la kazi duniani, ILO, linakadiria kuwa kupitia utumwa wa kisasa zaidi ya watu milioni 40 wametumbukia kwenye mfumo huo.

TAGS: ILO, ICAO, OHCHR, Usafirishaji haramu