Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani wa MINUSMA watunzwa medali za UN

Katibu Mkuu UN António Guterres anahudhuria sherehe huko Bamako, Mali, akiwaenzi walinda amani wote waliofariki katika Siku ya Kimataifa ya Walinzi wa Amani UN .
Picha ya MINUSMA/Olivier Salgado Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,António Guterres ahudhuria shereh mjini Bamako, Mali ametoa heshima zake kwa walinda amani katika siku ya kimataifa ya walinda amani.

Walinda amani wa MINUSMA watunzwa medali za UN

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ametumia siku yake nzima leo na walinda amani wa ujumbe wa umoja huo mjini Bamako nchini Mali, MINUSMA ambapo amewatunza medali walinda amani wawili wa ujumbe huo.

Kabla ya kuvisha medali hizo, Katibu Mkuu alishiriki tukio maalum la kumbukizi ya walinda amani kwenye kambi ya MINUSMA kwa kuweka shada la maua katika mnara wa ujumbe huo ulio na majina ya walinda amani waliouawa wakiwa kazini.

 

Katibu Mkuu UN António Guterres akiweka shada la maua katika sherehe ya ukumbusho huko Bamako, Mali, kwa ajili ya walinda amani waliofariki wakihudumu katika MINUSMA.
Picha ya UN/Marco Dormino Katibu Mkuu aweka shada la maua katika mnara wa walinda amani waliouawa wakiwa katika kazi za MINUSMA. Sherehe imefanyika katika kambi ya MINUSMA Bamako.

 

MINUSMA ni operesheni inayoongoza kwa kushambuliwa mara kwa mara na mwaka jana pekee walinda amani 21 waliuawa pamoja na raia 7.

Guterres amesema,

walinda amani wamedhihirisha ujasiri wao

walinda amani, mmedhihirisha  kuwa mnaweza kujitolea kwa dhati   

hata kwa niaba ya wenzenu wengi, jambo ambalo ndilo kilele cha kujitolea kulinda maisha ya raia wa Mali. Nataka kuwapongeza kwa hilo na kujitolea  kwenu na kusema najivunia kufanya kazi nanyi.”

Katibu Mkuu amesema walinda amani ndio alama ya Umoja wa Mataifa.

Waliovishwa medali ni Olufunmilayo Ajibike Amodu,  kutoka Nigeria ambaye ametambuliwa kuwa afisa bora pamoja na Meja Mohammed Badrul Ahsan Khan, kutoka Bangladesh.

Bw Guterres anaandamana na Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF Henrietta H. Fore na Atul Khare ambaye ni msaidizi wa Katibu Mkuu kwenye operesheni za amani mashinani.

Katibu Mkuu UN Antonio Guterres na Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita katika mkutano na waandishi wa habari mjini Bamako.
Picha na UN /Harandane Dicko Katibu Mkuu Antonio Guterres (kushoto) amelakiwa uwanja wa ndege wa kimataifa na rais wa Mali, Ibrahim Boubacar Keita

 

Awali Katibu Mkuu alilakiwa kwenye uwanja wa ndege na Rais Ibrahim Boubacar Keita wa Mali ambapo watakuwa na mazungumzo baadaye leo.

Kesho Jumatano Bwana Guterres anatarajiwa kutembelea maeneo ya mikoani nchini Mali ili kukutana na viongozi wa mamlaka mbalimbali, wakiwemo wawakilishi wa wanawake, vijana na viongozi wa kidini pamoja na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.