Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia wa Sudan Kusini asimulia alivyobakwa baada ya mumewe kuuawa

Picha:MONUSCO
Ubakaji na ukatili wa kingono ni ukiukaji wa haki za binadamu

Raia wa Sudan Kusini asimulia alivyobakwa baada ya mumewe kuuawa

Amani na Usalama

Hali bado si shwari kwenye jimbo la Unity nchini Sudan Kusini, jambo linalofanya maelfu ya raia wa kukimbia mapigano huku wakikumbwa na madhila ikiwemo kubakwa. 

Hapa ni katika kaunti ya Mayendit, jimbo la Unity nchini Sudan Kusini, raia wengi wao wanawake na waatoto wakiwa wamesaka hifadhi kwenye kituo cha muda cha hifadhi wa raia cha Umoja wa Mataifa.

Wamefika hapa baada ya kujificha vichakani kwa muda wakikimbia

mapigano jimboni humo baina ya pande kinzani.

Miongoni mwao ni Nyapuka Riak Kai  na mtoto wake mwenye umri wa miaka tisa.

Mumewe Nyapucka aliuawa wakati wa mapigano  na sasa amebakia hajui la kufanya na baya zaidi ni madhila aliyopitia,  “tumekuja hapa kwa sababu adui walishambulia eneo letu na wakamuua mme wangu, wakachoma nyumba zetu na hata watu wengine waliteketea wakiwa  ndani ya nyumba zao. Wanawake wengi walibakwa, na mimi pia nilibakwa na wanaume 10, lakini niliweza kutoroka na mtoto wangu.”

Ingawa amepata makazi ya mudam bado hajui jinsi gani atamlinda mtoto wake  au jinsi ya kupata chakula wanachokihitaji mno ili waweze kuishi.

Mahali hapa hamna vyoo wala mahali pa kuogea na hali hiyo inatishia kusababisha magonjwa.

Takriban watu 2000 wamejibanza kwenye kambi hii ya muda na asilimia 80 ni wanawake na watoto.

Tom Taisi ni afisa wa misaada wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS. anasema, “kwa sasa kuna hatua zinazochukuliwa na watoaji misaada pamoja na UNMISS kuongeza msaada kwa watu wanaosaka amani pamoja na wengine walioko katika eneo hili la muda la hifadhi au TPA.”