Mkakati mpya wa WHO kuokoa watu milioni 29 ifikapo 2023

23 Mei 2018

Wajumbe wa mkutano wa Baraza Kuu la shirika la afya ulimwenguni, WHO wameridhia mpango mpya wa mkakati wa  miaka mitano wenye lengo la kusaidia kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu SDGs.

Wajumbe wamefikia uamuzi huo hii leo huko Geneva, Uswisi ambapo mkazo ni lengo namba 3 la SDGs la kuhakikisha afya bora na ustawi wa kila mtu ifikapo mwaka 2030.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk. Tedros Ghebreyesus, amewaeleza wajumbe hao kuwa mpango unaonekana kuwa na matumaini makubwa lakini ni lazima uwe hivyo.

Mpango huo wa kimkakati unalenga malengo madogo matatu ambayo ni, mosi, kuhakikisha ifikapo mwaka wa 2023, watu zaidi ya  bilioni moja  wawe wananufaika na huduma ya afya kwa wote, pili, watu bilioni moja wengine wawe wanalindwa dhidi ya dharura za kiafya na tatu watu wengine bilioni moja wawe wanajivunia afya bora na ustawi.

WHO inakadiria kuwa kwa kutekeleza mpango huo, inaweza kuokoa maisha ya watu millioni 29.

Wakigusia mpango huo, wajumbe wamebaini kuwa ili utekelezeke ni sharti  WHO ifanye mabadiliko makubwa ya kimkakati, kama kuboresha suala la afya ya umma, kumulika jinsi unavyotekelezwa  katika mataifa mbalimbali na pia kuhakikisha kuwa watu wanaweza kupata taarifa za uhakika kuhusu masuala yanayoathiri afya ya binadamu.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud