Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya vituo vinavyotibu Fistula Tanzania vyaongezeka

Bi. Hadija, mkazi wa Morogoro nchini Tanzania alipata Fistula miaka 25 iliyopita. Hata hivyo akiwa na umri wa miaka kama 55 alifanyiwa upasuaji na sasa amepona kabisa ugonjwa umesalia historia. (Picha:UNFPA-Tanzania/Video capture)

Idadi ya vituo vinavyotibu Fistula Tanzania vyaongezeka

Afya

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kutokomeza fistula, Umoja wa Mataifa nchini Tanzania umesema kuna matumaini makubwa ya kuondokana na adha hiyo ya kiafya kwa wanawake na wasichana licha ya changamoto zilizopo.

Ujumbe wa mwaka huu ni kutokumwacha nyuma mwanamke yeyote anayekabiliwa na tatizo hilo la kiafya linalotokana na kuwepo kwa tundu kati ya kibofu cha mkojo na njia ya uke au hata na njia ya haja kubwa.

Fistula husababishwa na uzazi pingamizi ambapo Afisa wa afya ya mama na mtoto wa shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu, UNFPA nchini humo Furaha Mafuru ameiambia idhaa hii kuwa uelewa mdogo ni miongoni mwa changamoto kuu za kutatua shida hiyo inayoweza kutibika.

Ukosefu wa vituo vya matibabu ni changamoto nyingine lakini Bi. Mafuru amesema UNFPA inasaidia kuboresha vituo na idadi imeongezeka.

UNFPA inasema nchini Tanzania hivi sasa kuna wanawake kati ya 10,000 na 20,000 wanaougua Fistula na kwamba kila mwaka kuna wagonjwa wapya 3000 ambapo ni 1300 pekee ndio wanapata tiba.