Haki za binadamu ziko mashakani kwa sasa-Zeid

Zeid Ra'ad Al Hussein mkuu wa kamisheni ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, akitoa hotuba mjini Vienna, Austria wakati wa kuadhimisha miaka 25 ya mkutano wa dunia kuhusu haki za binadamu
Picha ya UNIS Vienna/Lilia Jiménez-Ertl
Zeid Ra'ad Al Hussein mkuu wa kamisheni ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, akitoa hotuba mjini Vienna, Austria wakati wa kuadhimisha miaka 25 ya mkutano wa dunia kuhusu haki za binadamu

Haki za binadamu ziko mashakani kwa sasa-Zeid

Amani na Usalama

Dunia inarudi nyuma katika masuala ya haki za binadamu  na misingi yake inavurugwa kila upande wa dunia hii, ameonya  Jumanne, afisa wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa,na kumhimiza kila mtu popote alipo kuonyesha  azma ya kujitolea katika kulinda haki hizo.

Katika hotuba, inayoonekana kama kali kuadhimisha miaka 25 ya mkutano wa dunia kuhusu haki za binadamu ambayo ilitilia mkazo wa hali ya haki za binadamu ambazo ni za wote  hazibadiliki na kuwa na uhusiano,  mkuu wa tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, Zeid Ra’ad Al Hussein, amesema kuwa baada ya robo karne kupita, ulimwengu unaonekana kama, unageuza  mkondo.

Katika mkutano wa 1993, mataifa 171 yalipasisha tamko la Vienna lenye mpango tekelezi, wa kuimarisha haki za binadamu duniani kote. Hiyo ilionekana kwa wengi, kama muhimili wa haki zote za wakati wa baada ya vita baridi.

Pia mkutano huo ulianzisha mchakato wa kuunda ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, kwa kifupi OHCHR ,inayoongozwa kwa sasa na Bw Zeid mwenyewe.

Akihutubia mkutano huo Jumanne, afisa huyo wa haki za binadamu kutoka Umoja wa Mataifa, amesema kuwa kuna kurudi nyuma hadi  wakati ambapo ubaguzi wa rangi pamoja na chuki dhidi ya wageni, vikichochea, kimakusudi, chuki na ubaguzi miongoni mwa  umma, kwa kisingizio  cha demokrasia na utawala wa sheria.

 Ameonya kuwa, sanasana katika bara la Ulaya, vyama vya kisiasa vinavyoegemea sana katika misingi ya kikabila vinaongezeka kila mara katika mataifa mengi na vinachochea chuki pamoja na mgawanyiko.

Endapo vyama hivyo vikishika madaraka, kimakusidi husambaza  mtazamo wa uongo kuwahusu wahamiaji pamoja na wanaharakati wanaotetea haki za binadamu.

Karibu kila mahali, Ulaya nzima, chuki dhidi ya wahamiaji imepenyeza hata katika  vyama vikuu na kupoteza dira ya mwelekeo kisiasa  kuelekea ghasia na mateso.

Leo si wakati wa kufumbia macho

Akibaini vitisho dhidi ya haki za binadamu duniani kote, ambavyo sasa  havichukuliwi kama kipaumbele bali kuchukuliwa kama kitu cha chini sana, amemuomba kila mtu kusimama kidete kutetea kile kinachiowalisha tamko la Vienna.

“Tunahitajika kutumia maadhimisho haya kuanza kuihamasisha jamii kulinda haki za binadamu kwa dhati,” amesema Bw Zeid, huku akikariri haja ya kuweka wazi alichoita, “haki za binadamu muhimu kwa maisha ya kawaida ya mwanadamu pamoja na  mustakbala wa binadamu wenzetu.”

Ameongeza kuwa “Hakuna cha kupoteza muda sasa. Acha hii iwe ndio kichocheo, ili tamko la Vienna lichomoze sio kama  kitu cha mambo ya kale kinachozeeka , bali kama mshika bendera wa vuguvugu lenye nia ya kujenga amani na maendeleo” amesema.