Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utoaji chanjo dhidi ya Ebola waendelea Mbandaka

Chanjo ya ebola(Picha ya WHO/M. Missioneiro)

Utoaji chanjo dhidi ya Ebola waendelea Mbandaka

Afya

Utoaji chanjo dhidi ya Ebola ukiendelea huko jimbo la Equateur nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, imeelezwa kuwa idadi ya washukiwa wa Ebola sasa imefikia 28.

Idadi hiyo imetangazwa hii leo huko Geneva, Uswisi na msemaji wa shirika la afya ulimwenguni, WHO Tarik Jasarevic wakati akizungumza na waandishi wa habari, akisema ni kati ya visa 51 vilivyoripotiwa tangu kuzukwa kwa ugonjwa tarehe 8 mwezi huu..

Bwana Jasarevic pamoja na kusema kuwa idai ya vifo imefikia 27 baada ya mgonjwa mwingine kufariki dunia, amezungumzia pia utoaji wa chanjo ya Ebola kwenye mji wa Mbandaka,“Watu 33 walipata chanjo jana huko Mbandaka. Watu hao ni wahudumu wa afya na watu wengine wachache kwenye jamii huko Mbandaka. Chanjo inaendelea kutolewa leo. Huko Bikoro, wadau wetu kutoka MSF watahusika kwenye chanjo na tunatumai hii itaanza baadaye wiki hii au wiki ijayo pindi maandalizi yatakapokamilika. Utoaji chanjo unaongozwa na Wizara ya Afya ya DR Congo.”

Bwana Jasarevic amesema utoaji wa chanjo huko Bikoro una changamoto zaidi kutokana na miundombinu akisema, “Kupata hizo chanjo, kupata majokofu na kuwa na mafuta ya kutosha ya kuwezesha majokofu haya kufanya kazi kwenye maeneo yasiyo na  umeme. Unahitaji wahudumu wabobezi kwenye kutoa chanjo ili waweze kufahamu fika kile wanachopaswa kufanya, jinsi ya kupata ridhaa na kutambua nani anafaa kupata chanjo, watu waliomzingira na wengine na wengine, ili yote hayo yafanyike katika kipindi kifupi.”

Chanjo inayotolewa kwa mfumo wa mzunguko yaani ikilenga wagonjwa na watu waliokuwa karibu nao inaitwa , Zaire Ebola virus na ilikuwa na mafanikio makubwa huko Guinea.

Mlipuko wa mwaka huu wa Ebola nchini DRC ni wa 9 tangu mwaka 1976.