Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kaunti ya Meru yaonyesha mfano kusaidia vijana

Vijana wakishiriki kilimo nchini Kenya.(Picha:IFAD/Video capture)

Kaunti ya Meru yaonyesha mfano kusaidia vijana

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kaunti ya Meru nchini Kenya imezindua mpango wa miaka 5 wenye lengo la kuleta upya matumaini kwa vijana waliopoteza matumaini ya kujipatia kipato baada ya Muungano wa Ulaya kupiga marufuku bidhaa ya miraa yenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 6.

Mpango  huo umewekwa bayana wakati wa mkutano  wa siku mbili ulioandaliwa mjini Meru kwa ushirikiano kati ya shirika la Umoja wa Mataifa la makazi- UN-habitat na Kaunti ya Meru, chini ya kauli mbiu, mwezeshe kijana, wezesha mustakhbali wao.

Mpango huo ulizinduliwa mwezi uliopita na ni wa kwanza wa aina yake nchini Kenya ambapo vijana 1000 kutoka wadi za kaunti ya Meru walichukuliwa na katika kipindi cha mwaka mmoja watapatiwa mafunzo katika nyanja kama vile kilimo, huduma za afya na ustawi wa miji.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa UN-Habitat Dkt. Aisa Kacyira ameunga mkono mpango huo akieleza utayari wa shirika lake kusaidia harakati za vijana za kuendeleza ujumuishi na ushirikishwaji wao katika utawala bora kama njia mojawapo ya kuimarisha ustawi wa vijana.

Naye mkuu wa kitengo cha vijana UN-Habitat, Douglas Raga, amesema kuwa eneo la   Meru linakua kwa kasi mno na vijana wengi wanatoka mashambani wakimiminika katika sehemu za miji wakitafuta ajira na elimu.

Akaongeza kuwa UN-Habitat inashirikiana na kaunti ya Meru kusaidia vijana katika maisha yao kwa kuwasaidia walio maskini kwakuwapatia maelekezo kupitia mafunzo pamoja na misaada.

Naye mtaalam wa masuala ya vijana katika ofisi ya UN-Habitat Linus Sijenyi, amesema kuwa matokeo ya mkutano huo yatatumiwa kama mfano wa kuigwa na kaunti zingine nchini Kenya.

Mkutano umewawezesha vijana wa kike na kiume kutambua jinsi ya kujihusisha katika kuboresha  maisha yao ya kawaida pamoja na ya kiuchumi katika Kaunti ya Meru.