Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chanjo dhidi ya Ebola yaanza kutolewa Mbandaka

Uandaaji wa chanjo ya ebola katika maabara hospitali ya Donka, Conakry, Guinea
WHO/S. Hawkey
Uandaaji wa chanjo ya ebola katika maabara hospitali ya Donka, Conakry, Guinea

Chanjo dhidi ya Ebola yaanza kutolewa Mbandaka

Afya

Chanjo dhidi ya ugonjwa wa Ebola imeanza kutolewa hii leo kwenye jimbo la Equateur nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Shirika la afya ulimwenguni WHO pamoja na wadau wanashirikiana kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa huo ambao tangu ulipuke tarehe 8 mwezi huu wa Mei jimboni humo umesababisha vifo vya watu 26 kati ya visa zaidi ya 45 vilivyoripotiwa.

WHO inasema chanjo hiyo ambayo bado iko kwenye majaribio, inaitwa Zaire Ebola virus na ilikuwa na mafanikio makubwa huko Guinea.

Dkt. Peter Salama, Naibu Mkurugenzi  Mkuu wa WHO masuala ya dharura anafafanua kuhusu utoaji wa chanjo hiyo akisema kuwa, inaitwa chanjo kwa mfumo wa mzunguko kwa sababu hii si kampeni ya kawaida ya chanjo ambayo unapatia chanjo wakazi wote wa eneo fulani. Hii ina walengwa.

"Kimsingi unabaini mgonjwa, halafu unabaini watu wote waliokuwa karibu na mgonjwa huyo, na wengine waliokuwa karibu na hao, wakiwemo wahudumu wa afya na hiyo inakupatia mzunguko uliomzigira mgonjwa.”

Utoaji wa chanjo hiyo unafanyika kwa utaalamu mkubwa kwa usaidizi wa wataalamu kutoka Guinea ambako utoaji wa chanjo hiyo wakati wa mlipuko wa Ebola  ulikuwa wa mafanikio makubwa.

Awali Ebola iliripotiwa kwenye mji wa Bikoro huko jimboni Equateur lakini hofu ilitanda zaidi baada ya WHO kubaini visa vya Ebola mjini Mbandaka jimboni humo, hali iliyotia shaka uwezekano wa ugonjwa huo kuenea kwa kasi.