Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Intaneti yaokoa maisha ya wakimbizi Niger

Picha na (NAMS)
Wasichana wakitumia simu ya mkononi (Picha:UM)

Intaneti yaokoa maisha ya wakimbizi Niger

Msaada wa Kibinadamu

Huduma ya intaneti iliyofungwa katika kambi ya wakimbizi huko jimbo la Diffa, mashariki mwa Niger imeanza kuzaa matunda kwa mashirika ya misaada na wakimbizi ambao wote wananufaika na huduma ya simu na intaneti 

Hapa ni katika kambi ya Sayam Forage, jimboni Daffa ambako kwa muda mrefu huduma ya mawasiliano ilikuwa kikwazo.  

Hata hivyo shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi UNHCR, kwa msaada wa wahisani kutoka  Luxembourg walifanikiwa kufunga mitambo ya intaneti  ili kutatua tatizo la mawasiliano .

Ikipatiwa jina la Emergency.lu, huduma hiyo imekuwa msaada mkubwa wa mawasiliano kwenye kambi hii yenye zaidi ya wakimbizi laki mbili.

Alphonse Munyaneza ni mkuu wa ofisi ya UNHCR kusini mwa jimbo la Diffa,

Sauti ya Alphonse Munyaneza

 Sayam Forage ni kambi iliyoko katika mazingira magumu mno. Inapatikana katikati mwa jangwa. Ukifika Sayam Forage,utafikiri watu   waliamua kufungua kambi ya wakimbizi katikati mwa jangwa. Hakuna simu, hali ya hewa ni joto kali sana. Hivyo upatikanaji wa mtandao wa intaneti unakupa uhakika katika ufanisi wa kazi na huduma zetu .

Upatikanaji wa intaneti kambini hapa unarahisisha pia huduma kama vile za afya, vitambulisho kwa ajili ya  wakimbizi na pia  sekta ya elimu kama anavyoeleza Alessandra Morelli, mwakilishi wa UNHCR Niger.

Sauti ya Alessandra Morelli

“Mpango wa huduma ya mtandao, unawapa washirika uwezo wa kuzungumza lugha moja, na kuwa na nia  katika shughuli zinazotakiwa kupewa kipaumbele. Inawajumuisha wote, na ni kupitia ujumuishwaji huo ndipo tunaweza kuwa na uhakika kuwa hakuna anayeachwa nyuma.”

Kupitia huduma hii ya intaneti mashirika ya misaada ya kibinadamu, yanapata fursa ya kuwasiliana na asasi za kiraia, serikali na mashirika mengine katika nyakati za dharura, majanga na mahitaji mengine muhimu ya kibinadamu.