Viongozi wa Sudan Kusini wekeni maslahi ya watu wenu mbele -UN
Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini wa UNIMISS amewahimiza viongozi nchini humo kuweka maslahi ya watu wao kwanza na kutumia wakati huu ili wasikilizane waweze kuleta amani ya kudumu.
Mkuu wa UNIMIIS,David Shearer, ameyasema hayo mjini Addis Ababa katika mkutano wa ngazi za juu wa jukwa la kuongeza matumaini ambapo ameeleza madhila yanayowakuta watu aliowashuhudia alipozuru jimbo la Unity nchini Sudan Kusini hivi majuzi, ambako mapigano yanaendelea.
“Nimeona uharibifu. Nimeona ‘tukuls’ zilizochomwa. Nimesikia wanawake na wasichana ambao walibakwa,watu waliouawa, na wengine maelfu ambao waliojificha katika vinamasi wakitoroka kuuawa’’, amesema.
David Shearer, ambae pia ni mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesema kuwa watu aliozungumza nao walimuomba kupeleka ujumbe mzito katika mazungumzo hayo.
“Kwa niaba ya watu hao, nawaombeni, nawasihi, na kuhitaji kutoka kwenu, mtafute njia ya kuelewana, mpatane ili mpate amani na kuweza kusaidia watu hao niliowakuta, waweze kuishi maisha mazuri.”
Jukwa hilo ni nafasi kwa pande zote husika kuja pamoja kuendeleza mazungumzo ya amani kuhusiana na mkataba wa kusitisha uhasama waliosaini miezi mitano iliyopita mjini Addis Ababa
Yeye mwenyekiti wa baraza la mawaziri wa IGAD Dr, Workneh Gebeyehu, amesema kuwa baraza lake liko tayari kuchukulia hatua dhidi ya yeyote atakaekwenda kinyume na mkataba wa Addis Ababa.IGAD ni kundi linalojumuisha mataifa nane ya Afrika katika masuala ya kiuchumi.