Watoto wengine zaidi ya 200 waachiliwa na waasi Sudan Kusini:UNICEF

18 Mei 2018

Kwa mara ya tatu mwaka huu watoto wengine zaidi ya 200 wameachiiliwa Alhamisi na makundi ya waasi nchini Sudan Kusini.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF tangu mwanzoni mwa mwaka huu sasa jumla ya watoto 806 wameachiliwa na wengine zaidi wanatarajiwa katika miezi ijayo ili idadi kufikia zaidi ya watoto 1000.

Mahimbo Mdoe ambaye ni mwakilishi wa UNICEF Sudan Kusini amesema kila wakati mtoto anapoachiliwa na kuweza kurejea kwa familia yake ni chanzo cha matumaini makubwa kwa mustakhbali wake na taifa lake.

Askari watoto nchini Sudan Kusini wakabidhiwa kwa UNICEF
UNICEF Sudan Kusini/Marinetta Peru
Askari watoto nchini Sudan Kusini wakabidhiwa kwa UNICEF

Ameongeza kuwa matumaini yao ni kuendelea kuachiliwa kwa watoto hao hadi kuwe hakuna tena mtoto hata mmoja kwenye vyeo vya makundi ya waasi.

Katika hafla maalumu ya zoezi hilo , watoto walipokonywa silaha na kukabidhiwa mavazi ya kiraia ,  sasa hatua inayofuata ni kufanyiwa vipimo vya kitabibu, kupatiwa ushauri nasaha na msaada wa kisaikolojia kama sehemu ya kuwarejesha tena katika maisha ya kawaida, mpango unaoendesha na shirika la UNICEF na washirika wengine.

Watoto hao wakishakabidhiwa kwa familia zao watapewa msaada wa miezi mitatu wa chakula , pia watapewa mafunzo ya kiufundi yatakayowawezesha kusaidia kuinua kipato cha familia zao na uhakika wa chakula.

UNICEF na wadau wengine watahakikisha pia watoto walioachiliwa wanapatiwa fursa ya elimu kulingana na umri wao.

Sherehe za awali zilifanyika Februari na Aprili mwaka huu mjini Yambio Kusini mwa nchi hiyo ambapo awamu ya kwanza watoto 348 waliachiliwa na kisha wengine 248 wakafuatia.

Bwana mdoe amesema kuachiliwa leo kwa watoto hao ni kuanza safari ndefu ya kurejea katika maisha ya kawaida na watahitaji msaada wa kila aina kufanikisha safari hiyo.

Watoto 210 walioachiliwa leo ni pamoja na wasichana watatu, na sehemu kubwa wametoka kwenye kundi la upinzani la SPLA-IO na wengine wanane wakihusishwa na kundi la ukombozi wa kitaifa la NSF.

Tatizo la askari watoto lipo pia DRC.Umoja wa Mataifa wataka mataifa yote kuafiki kutowatumia watoto katika migogoro ya kijeshi.
UN Photo/Marie Frechon
Tatizo la askari watoto lipo pia DRC.Umoja wa Mataifa wataka mataifa yote kuafiki kutowatumia watoto katika migogoro ya kijeshi.

Watoto wanaokadiriwa kufikia 19,000 wanaendelea kuhudumu katika vyeo mbalimbali katika vikosi vyenye silaha na makundi ya waasi Sudan kusini. UNICEF imerejea kutoa wito wa kuzitaka pande zote katika mzozo nchini humo kukomesha uingizaji jeshini watoto na kuwaachilia wale wote walio katika vikosi vyao.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter