Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utipwatipwa na uvutaji sigara vina uhusiano

Wengine wakiwa wamesimama karibu, mtoto analishwa na mamaye katika uwanja wa michezo ya watoto Disney World huko Orlando, Florida, nchini Marekani. Utipwatipwa ni tatizo kubwa nchini humo. Picha: UNICEF/Toutounji

Utipwatipwa na uvutaji sigara vina uhusiano

Afya

Utafiti mpya umebaini kuwa watu ambao kwao unene au utipwatipwa ni asili au jambo la kurithi kwenye familia zao wako hatarini zaidi kuwa wavutaji sigara, na wanaweza kuvuta sigara kwa kiwango kikubwa zaidi.  Grace Kaneiya na ripoti kamili.

(Taarifa ya Grace Kaneiya)

Wanasayansi kupitia utafiti huo uliofanywa na taasisi ya utafiti wa saratani duniani, IARC, taasisi tanzu ya WHO,  wamesema kuna jeni mpya 70 zilizobainika na zinaonyesha uhusiano kati ya utipwatipwa na uvutaji sigara.

Dkt. Paul Brennan kutoka IARC amesema jeni hizo zimejikita kwenye seli za ubongo.

(Sauti ya Dkt. Paul Brennan)

 “Baadhi yao zinaonyesha uhusiano mkubwa na ubongo, yaani ni jeni zinazohusika na mfumo wa mawasiliano wa seli. Na hii inadokeza kuwepo kwa vigezo vya pamoja vya mfumo wa mawasiliano ya seli unaoelezea uhusiano wa pamoja kati ya utipwatipwa na uvutaji sigara na iwapo unataka kuacha au la.”

 Dkt. Brennan akaelezea ni vipi utafiti utasaidia kampeni dhidi ya uvutaji sigara na utipwatipwa ambavyo vyote husabaisha magonjwa.

 (Sauti ya Dkt. Paul Brennan)

 “Tunapaswa kuzingatia mambo haya mawili kwa pamoja. Hivyo unapofikiria kuzuia matumizi ya tumbaku, tunatakiwa pia kufikiria nafasi ambayo utipwatipwa inaweza kuchangia kwa mtu kuanza kuvuta sigara, na ugumu wanaopata watu kuacha sigara na umuhimu wa iwapo utipwatipwa uzingatiwe katika kampeni hii.”