Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola yabainika mjini Mbandaka, WHO yaingiwa na hofu

Wahudumu wa afya wakijiandaa kushughulikia wanaoshukiwa kuwa na ugonjwa wa ebola hospitali ya Bikoro nchini DRC
UNICEF/Mark Naftalin
Wahudumu wa afya wakijiandaa kushughulikia wanaoshukiwa kuwa na ugonjwa wa ebola hospitali ya Bikoro nchini DRC

Ebola yabainika mjini Mbandaka, WHO yaingiwa na hofu

Afya

Shirika la afya ulimwenguni WHO lina hofu kubwa hivi sasa baada  ya mgonjwa wa Ebola kubainika maeneo ya mjini huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Serikali ya DRC imelitaarifu shirika hilo kuwa mgonjwa amebainika eneo la Wangata, moja ya kanda tatu za mji wa Mbandaka, mji wenye watu milioni 1.2 katika jimbo la Equateur.

Hadi kuripotiwa kwa kisa hiki wagonjwa wote na vifo vitokanavyo na Ebola kwenye jimbo hilo vilikuwa vimeripotiwa huko Bikoro, eneo lililo takribani kilometa 150 kutoka Mbandaka.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moeti amesema kupatikana kwa kisa cha Ebola maeneo ya mjini ni jambo la kutia hofu lakini WHO na wadau wanaimarisha msako wa watu wote waliokutana au kugusana na mgonjwa huyo huko Mbandaka.

Amesema WHO inapeleka wataalamu 30 kutekeleza operesheni hiyo huko Mbandaka na inashirikiana na Wizara ya afya ya DRC na wadau wengine kushirikisha jamii kwenye mbinu za kujikinga na kutibu Ebola pamoja na kutoa taarifa kuhusu visa vipya.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Gebreyesus amesema ingawa wana hofu, wana matumaini kwa kuwa hivi sasa wana vifaa na mfumo bora wa kuweza kuzuia kuenea na kukabili Ebola.

Hadi tarehe 15 mwezi huu wa Mei, wagonjwa 21 wamefariki dunia kutokana na Ebola huko DRC.

WHO KUWA NA KIKAO CHA DHARURA KESHO KUHUSU EBOLA

Wakati huo huo, shirika la afya ulimwenguni, WHO kesho Ijumaa litakuwa na kikao cha dharura kujadili iwapo itangaze mlipuko wa Ebola huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ni tishio la afya kwa umma duniani.

Kamati ya wataalamu wa WHO itaangalia iwapo ichukue hatua hiyo, jambo ambalo litachochea ushiriki zaidi wa jamii ya kimataifa katika kusaka rasilimali za kusaidia operesheni dhidi ya kuenea kwa ugonjwa huo.

Pindi milipuko ya magonjwa hatari inapotokea, WHO huunda kamati za dharura ikitolea mfano wakati wa mlipuko wa Zika huko Amerika ya Kusini mwaka 2016 pamoja na mlipuko wa Ebola huko Libera kuanzia mwaka 2014 hadi 2016 uliosababisha vifo vya watu wapatao 11,300.