Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu bilioni 2.5 wataishi mijini ifikapo 2050:UN Ripoti

Miji katika mataifa yanayoendelea kwa mfano Nairobi nchini Kenya yanaendelea kukua kwa kasi.
UN-Habitat/Julius Mwelu
Miji katika mataifa yanayoendelea kwa mfano Nairobi nchini Kenya yanaendelea kukua kwa kasi.

Watu bilioni 2.5 wataishi mijini ifikapo 2050:UN Ripoti

Masuala ya UM

Ifikapo mwaka 2050 inakadiriwa kuwa watu wawili kati ya watatu watakuwa wanaishi mijini kwa mujibu wa ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo, ikiainisha haja ya kuwa na mipango miji endelevu na huduma muhimu za jami.

 

Makadirio hayo yaliyotolewa na idara ya uchumi na masuala ya kijamii ya Umoja wa Mataifa (DESA), yanamaanisha kwamba takriban watu bilioni 2.5 wataongezeka katika maeneo ya mijini katikati ya karne hii.

Ripoti hiyo inasema nchi nyingi zitakabiliwa na changamoto za kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya idadi kubwa ya watu mijini. Idadi kubwa inatarajiwa zaidi katika baadhi ya nchi za Asia na Afrika ambapo kwa pamoja nchi za India, China na Nigeria zitashikilia asilimia 35 ya matarajio ya idadi hiyo kati ya mwaka 2018 na 2050, huku India pekee ikitarajiwa kuongeza wakazi milioni 416 mijini, ikifuatia na China milioni 255 na Nigeria milioni 189.

Ripoti pia inakadiria kwamba ifikapo 2030  kutakuwa na miji 43 iitwayo majiji makubwa ikiongezeka kutoka 31 ya hivi sasa ambayo yoye ina watu zaidi ya milioni 10 kila mmoja na mingi itakuwa katika mataifa yanayoendelea.

Na ifikapo mwaka 2028 Delhi mji mkuu wa India ndio utakuwa mji wenye idadi kubwa kabisa ya watu duniani. Hivi sasa Tokyo Japan ndio inayoshika usukani kwa kuwa na watu milioni 37 ikifuatiwa na Delhi milioni 29, na Shangai milioni 26.

Miji mingine yenye watu wengi duniani ni Mexico City na Sao Paulo yote ikiwa na watu milioni 22 kila mmoja.

Ripoti hiyo ya DESA inasema changamoto kubwa mijini itakuwa nyumba, usafiri, nishati, miondombinu mingine ya msingi, ajira na huduma za msingi kama elimu na, afya.