Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mienendo ya watu yafuatiliwa ili kudhibiti Ebola DRC

Umakini unapaswa kuendelea ili kuhakikisha Ebola inatokomezwa. Picha ya UNICEF/NYHQ2014-3000/James

Mienendo ya watu yafuatiliwa ili kudhibiti Ebola DRC

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM nalo limejumuika katika kusaidia kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa Ebola huko jimbo la Equateur nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

IOM inafuatilia mienendo na kukusanya taarifa za watu wanaoingia na kutoka jimboni humo kama njia mojawapo ya kusaidia wahudumu wa afya kufahamu ni maeneo yenye misafara mingi ili waimarishe hatua za kinga na uchunguzi.

Mkuu wa IOM huko DRC Jean-Phillipe Chauzy amesema wanachukua pia hatua za kinga na udhibiti wa maambukizi ya Ebola maeneo ya mpakani, maeneo ya ibada  ambako watakuwa wanatoa elimu ya kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.

Amesema wanaanzisha pia mfumo ambao kwao utawezesha wasafiri wanaobainika kuwa na Ebola waweze kuelekezwa au kupelekwa kwenye vituo vya matibabu.

Bwana Chauzy amesema IOM wamechukua hatua hizo kwa kuzingatia kwamba Ebola haitambui mipaka na hivyo bila kufanya hivyo itakuwa rahisi kuenea kwenye siyo tu majimbo ya DRC bali pia nchi jirani.

Wizara ya Afya ya DRC ilitangaza mlipuko wa Ebola kwenye jimbo la Equateur tarehe 8 mwezi huu wa Mei ambapo hadi sasa kati ya visa 21, wagonjwa 17 wamefariki dunia huko Bikoro.

Yaelezwa kwamba tangu wakati huo idadi ya visa vinavyoshukiwa kuwa ni Ebola nayo imeongezeka, ingawa kwamba haikutajwa.

Huu ni mlipuko wa 9 wa Ebola nchini DRC tangu mwaka 1976.