Paneli za sola huko Morocco ni mfano wa kuigwa- Guterres

16 Mei 2018

Changamoto kubwa duniani kwa sasa ni mabadiliko ya tabianchi ambayo ni tishio kubwa kwa  maisha ya viumbe hususan uhai wa mwanadamu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema hayo leo akihutubia mkutano kuhusu hali ya hewa mjini Vienna Austria uliofanyika kuangazia usaidizi unaotakiwa ili kufanikisha mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi.

Bwana Guterres amenukuu takwimu zionyeshazo kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wakazi duniani wanaishi kwenye mazingira yanayoathiri afya zao.

Kwa mantiki hiyo Bwana Guterres ametaka kasi zaidi za kutekeleza mkataba huo akitolea mfano nchi zilizochukua hatua kuzalisha nishati isiyo chafuzi.

Mathalani Morocco ambako amesema kuna eneo lenye ukubwa wa mji wa Paris lenye paneli za kukusanya mionzi ya jua ili kuzalisha nishati ya umeme.

Vilevile ameigusia China ambayo mwezi Julai mwaka jana ilifikia lengo lake la kuzalisha nishati ya jua ya gigawatti 105, na kusisitiza kuwa mwongo mmoja uliopita China ilikuwa na nishati ya jua ya megawatti 100 tu.

Bwana Guterres amesema huu ni wakati wa kuhakikisha dunia inapunguza ongezeko la nyuzi joto kutoka 2 hadi 1.5 katika kipimo cha selsiyasi.

Amewataka viongozi wa sekta binafsi kutangaza  ufadhili mpya wa miradi ya nishati safi.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud