Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauaji ya watoto Burundi katu hayakubaliki:UN

Mei 29, centia mwenye umri wa miaka 12, akitembea katika jimbo la kirundo, Burundi
Picha:UNICEF/UNI186074/Nijimbere
Mei 29, centia mwenye umri wa miaka 12, akitembea katika jimbo la kirundo, Burundi

Mauaji ya watoto Burundi katu hayakubaliki:UN

Haki za binadamu

Umoja wa Mataifa umelaani vikali shambulio lililotokea mkoani Cibitoke nchini Burundi na kukatili Maisha ya watu 25 wakiwemo watoto 11.  Tupate maelezo zaidi na Grace Kaneiya

(TAARIFA YA GRACE KANEIYA)

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva Uswis msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF Christophe Boulierac, amesema Umoja wa Mataifa likiwemo shirika la UNICEF na ofisi ya haki za binadamu ya umoja wa mataifa wamesikitishwa sana  na shambulio hilo na kwamba wanaingiwa na hofu ya kuzuka kwa ghasia katika wakati huu wa maandalizi ya kura ya maoni inayotarajiwa kufanyika siku chache zijazo na kuongeza kwamba

(SAUTI YA BOULIERAC)

“Tukio hili laweza kuwa ndio mwanzo wa hali mbaya. Wanawake 10 na  watoto 11 ni miongoni mwa wahanga wa shambulio hilo ambapo watu wasiojulikana walishambulia kijiji cha Ruhamagara’’

Kijiji hicho kiko umbali wa kilomita 60 kutoka mji mkuu Bujumbura, duru mbalimbali zinasema watoto walilengwa kwa makusudi katika shambulio hilo lililtokea Mei 11. Mkurugenzi wa kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika wa UNICEF, Leila Pakkala, amesema daima watoto wanahitaji amani na kulindwa, na sio kushambuliwa hivyo UNICEF inaomba pande zote husika katika mgogoro huo, kuhakikisha kuwa zinaheshimu haki za watoto kuweza kuwa salama, na pia kuwalinda watoto dhidi ya ghasia zozote.

UNICEF imesema inaunga mkono juhudi za serikali za kuimarisha mfumo wa kulinda haki za watoto katika jamii kupitia kamati mbalimbali ili kuzuia tisho dhidi ya mustakhbali wa watoto hao.