Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mbinu rahisi na sahihi za uchunguzi wa magonjwa kuokoa maskini- WHO

Mhudumu wa Afya kutoka Mongolia akitoa huduma kwa mama na mtoto Darfur,Sudan(10 Disemba 2012)
Picha/ UN/Albert Gonzales Farran
Mhudumu wa Afya kutoka Mongolia akitoa huduma kwa mama na mtoto Darfur,Sudan(10 Disemba 2012)

Mbinu rahisi na sahihi za uchunguzi wa magonjwa kuokoa maskini- WHO

Afya

Shirika la afya ulimwenguni WHO limechapisha orodha ya vipimo vya lazima vya kubainisha magonjwa kama njia mojawapo ya kuboresha uchunguzi wa magonjwa hayo na matibabu yake.

Hatua hiyo ya WHO inazingatia ukweli kwamba watu wengi hususan kwenye nchi maskini wanashindwa kupata vipimo muhimu vya maradhi na hata wakati mwingine kupata majibu yasiyo ya kweli na kutibu magonjwa yasiyo sahihi.

Orodha hiyo ina vipimo 113 ambapo kati ya hivyo 58 vinahusisha uchunguzi wa damu au mkojo ilihali vipimo 55 vinalenga magonjwa kama vile Ukimwi, Kifua Kikuu, Malaria, homa ya Ini aina ya B na C pamoja na kaswende.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema baadhi ya vipimo hivyo vinaweza kufanyika hata kwenye vituo vya afya ambako hakuna huduma za umeme na hazihitaji wabobezi wa maabara. Vipimo vingine vinahitaji maabara zenye vifaa vya uwezo wa juu.

Dkt. Tedros amesema lengo ni kuweka mfumo ambao utafaa kwa nchi zote katika kuchunguza na kutoa tiba sahihi na pia kuhakikisha fedha zinatumika vyema.

Kwa kutoa orodha hiyo, nchi wanachama nazo zinapaswa kuboresha au kuandaa orodha zao za vipimo muhimu vya magonjwa na WHO iko tayari kusaidia nchi hizo katika kutekeleza mpango huo.